Wednesday, August 24, 2011

ZIARA YA MKE WA BALOZI WA MAREKANI MKOANI IRINGA KATIKA PICHA

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kushoto) akiagana na
Meneja wa Hospitali ya Aga Khan-Iringa, Bibi. Veronica James (kulia) nje ya Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa



Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma akibadilishana mawazo na Mke wa Balozi wa Marekani nchi Tanzania, Bibi. Jacquiline Lenhardf alipofika kumsalimia Kaimu Mkuu wa Mkoa Ofisi kwake

ZIARA YA MKE WA BALOZI WA MAREKANI MKOANI IRINGA KATIKA PICHA

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (kushoto),
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka (kulia) na
Afisa USAID-Tanzania, Bibi. Ludovica Tarimo (katikati)
katika picha ya pamoja mj ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Friday, August 19, 2011

…WAHIMIZWA KULA VYAKULA VYA ASILI

Wananchi wa Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili na kuachana na vyakula vya kisasa ili kujenga na kuboresha afya zao.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba (kulia) akila ugali wa mtama kwa mlenda na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Georgina Bundala (kushoto) akipata kikombe cha uji wa mtama katika kutoa hamasa ya ulaji wa vyakula vya asili.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba wakati akihamasisha ulaji wa vyakula vya asili katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji katika viwanja vya Johm Mwakangale, Uyole Mbeya.
Dumba amesema “nawahamasisha wananchi wote kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili ili kujenga na kulinda afya zao”.

Amesema ulaji wa vyakula vya asili unamfanya mtu kuwa na  nguvu na afya njema inayomfanya aweze kukabiliana na changamoto za kimaisha za kila siku na kutokuwa legelege.

Akiongea nje ya banda la maonesho la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, huku akiendelea kula ugali wa mtama kwa mlenda na simbilisi, Dumba amesema kuwa anajisikia furaha sana kwa sababu anapata “kitu roho inapenda” kwa sababu anapata mlo kamili.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Bundala katika uhamasishaji huo amesema viongozi wanawajibu wa kuwahamasisha wananchi wanaowaongoza kwa mifano katika yale wanayoyahubiri.

Huku nae akiwa anapata kikombe cha uji wa mtama ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa ubunifu huo wa kuleta vyakula vya asili kwa uhamasishaji na si maneno matupu.

Amesema wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususani mkoa wa Iringa wajenge utamaduni wa kulima zao la mtama ili kukabiliana na ukame unaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
TANI MIL 1.4 ZAONGEZEKA MAZAO YA CHAKULA NA BIASHARA IRINGA
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza kilimo cha mazao ya chakula na biashara hadi kufikia tani milioni 1.4 katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru.

Kaimu Katibu Tawala Msaidize, Sehemu ya Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Shenal S. Nyoni akifafanua jambo

Akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya kilimo katika miaka 50 ya Uhuru, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Shenal Nyoni katika Iringa Day iliyofanyika katika ukumbi wa JKT ndani ya uwanja wa John Mwakangale Uyole, Mbeya yanapofanyika maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Nyoni amesema “katika miaka ya 60 mkoa ulikuwa ukizalisha tani laki 3.05 za mazao hayo na hadi kufikia mwaka 2011 mkoa umefanikiwa kizalisha tani milioni 1.4”.

Amesema katika sekta ya uvuvi mkoa una mabwawa 4,167 yanayozalisha tani 1,449 za Samaki na kuuingizia shilingi bilioni 4.3 kwa mwaka.
Nyoni amesema kuwa mkoa pia ulishiriki katika mashindano ya mifugo ya Afrika Mashariki na kuchukua nafasi ya kwanza. Katika mashindano hayo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ndiyo ilichukua ushindi huo.

Akiongelea sekta ya viwanda amesema mkoa una viwanda vya kusindika na kuyaongezea mazao thamani. Mkoa una viwanda vikubwa vinne, viwanda vya kati 53 na 66 ni viwanda vidogo na mashine 1,992 za kusaga nafaka.

Awali akitoa salamu zake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amesema kuwa mkoa wa Iringa umefanikiwa kuzalisha chakula cha kuutosheleza mkoa kwa sehemu kubwa na kuonesha masikito yake kwa baadhi ya sehemu zinazokabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na upungufu mkubwa na ukame ulioyakabili baadhi ya maeneo hayo.

Amesema mkoa umalima mazao mengi yakimo mazao ya biashara kama mbao, chai, pareto, kahawa, alizeti na maua.

SUMBAWANGA YAPUNGUZA VIFO VYA AKINA MAMA

Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya akina mama hadi kufikia vifo 245 kati ya vizazi 100,000 mwaka 2010.

Hayo yamesemwa na Afisa Muuguzi wa Manispaa hiyo, A. Ngojo wakati akifafanua lengo namba mbili la Manispaa ya Sumbawanga la kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na ujauzito katika maonesho ya nanenane yaliyofanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole- Mbeya.

Ngojo amesema kuwa hadi kufikia Disemba 2010 Manispaa ya Sumbawanga iliweza kufikia lengo kwa kupunguza vifo hiyo toka vifo 263 kati ya vizazi 100,000 mwaka 2008 hadi kufikia vifo 245 kati ya vizazi 100,000 Disemba, 2010.

Amezitaja hatua zilizofikiwa kuwa ni kutoa motisha kwa wakunga wa jadi wanaowapeleka wajawazito kujifungua kwenye vituo vya afya na kupata huduma za kitaalamu. Hatua nyingine ameitaja kuwa ni kuongeza watumishi wenye ujuzi kwenye vituo vya huduma za afya toka 61% kwa mwaka 2008 hadi 91% kwa mwaka 2010.

Vilevile, kuongeza huduma za mkoba za uzazi wa mpango kutoka vituo 7 kati ya 15 (47%) kwa mwaka 2008 hadi kufikia vituo 11 (73%). Pia kuihamasisha jamii kuhusu uzazi wa mpango na kuimarisha huduma za vifaa ikiwa ni pamoja na magari ya kubeba wagonjwa.

Aidha, Manispaa hiyo imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wa umri chini ya mwaka mmoja kutoka 37 kati ya watoto 1000 mwaka 2008 hadi 17 kati ya watoto 1000 kufikia Disemba 2010.