Friday, August 19, 2011

…WAHIMIZWA KULA VYAKULA VYA ASILI

Wananchi wa Nyanda za Juu Kusini wametakiwa kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili na kuachana na vyakula vya kisasa ili kujenga na kuboresha afya zao.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sara Dumba (kulia) akila ugali wa mtama kwa mlenda na Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Georgina Bundala (kushoto) akipata kikombe cha uji wa mtama katika kutoa hamasa ya ulaji wa vyakula vya asili.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Sarah Dumba wakati akihamasisha ulaji wa vyakula vya asili katika maonesho ya Wakulima na Wafugaji katika viwanja vya Johm Mwakangale, Uyole Mbeya.
Dumba amesema “nawahamasisha wananchi wote kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili ili kujenga na kulinda afya zao”.

Amesema ulaji wa vyakula vya asili unamfanya mtu kuwa na  nguvu na afya njema inayomfanya aweze kukabiliana na changamoto za kimaisha za kila siku na kutokuwa legelege.

Akiongea nje ya banda la maonesho la Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, huku akiendelea kula ugali wa mtama kwa mlenda na simbilisi, Dumba amesema kuwa anajisikia furaha sana kwa sababu anapata “kitu roho inapenda” kwa sababu anapata mlo kamili.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Georgina Bundala katika uhamasishaji huo amesema viongozi wanawajibu wa kuwahamasisha wananchi wanaowaongoza kwa mifano katika yale wanayoyahubiri.

Huku nae akiwa anapata kikombe cha uji wa mtama ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa ubunifu huo wa kuleta vyakula vya asili kwa uhamasishaji na si maneno matupu.

Amesema wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hususani mkoa wa Iringa wajenge utamaduni wa kulima zao la mtama ili kukabiliana na ukame unaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

No comments:

Post a Comment