Saturday, December 1, 2012

UMASIKINI CHANZO CHA UKIMWI IRINGA




Hali ya umasikini na mila potofu zimeendelea kuchangia katika maambukizi ya VVU na UKIMWI katika Mkoa wa Iringa na kusababisha madhara makubwa kuanzia ngazi ya familia.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa akipata maelezo ya shughuli zinazofanywa na AMREF katika banda lao katika uwanja wa RUCO.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea banda la Ushauri nasaha na kupima VVU.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani katika Mkoa wa Iringa yalifanyika katika Chuo Kikuu kishiriki cha Ruaha.

Dkt. Christine amesema “hali ya maambukizi inatisha, madhara ya maambukizi ya VVU na UKIMWI ni makubwa hasa kutokana na sababu za umasikini, mila na desturi. Madhara haya ambayo huanzia katika ngazi ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watu ambao ni nguvu kazi ya Taifa la Tanzania”.

Amesema kuwa vifo vya wazazi husababisha kuongezeka kwa watoto yatima ambao wanahitaji msaada wa elimu, malazi, chakula na matibabu.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wake kwa kushirikiana na Halmashauri na mashirika yasiyo ya kiserikali wanatekeleza shughuli mbalimbali katika kukabiliana na kasi ya maambukizi ya VVU na UKIMWI.

Ameyataja maeneo maeneo ya ushirikiano kuwa ni katika kinga, huduma za kuzuia maambukizi mapya kwa watu ambao hawana maambukizi pamoja na wale wenye maambukizi kutokupata maambukizi mengine. Eneo lingine amelitaja kuwa ni tiba na huduma kwa walioathirika na janga la UKIMWI.

Dkt. Christine amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2011 hadi Juni 2012 jumla ya watu 130,882 walipata ushauri nasaha na kupima afya zao na kati yao 15,361 walikuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 10.5%.

Akiongelea utoaji wa huduma za upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma kwa mteja yoyote aendae hospitali akiwa anaumwa magonjwa mengine au kusindikiza, imesaidia sana kuwafanya watu wengi kujua hali ya afya zao kuhusiana na maambukizi ya VVU. Amesema katika jumla ya watu 23,184 waliopata huduma ya upimaji wa VVU baada ya kushauriwa na mtoa huduma,jumla ya watu 1,772 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU.

Aidha, huduma ya tohara kwa wanaume ni miongoni mwa njia zinazotumika katika kupunguza maambukizi ya VVU kwa wanaume.
Amesema kuwa huduma za tohara zimekuwa zikitolewa katika vituo vya huduma kama huduma ya kawaida. Mkuu wa Mkoa amesema “katika zoezi hilo jumla ya wanaume 113,076 wamekwisha tahiriwa katika mikoa ya Iringa na Njombe. Ili tohara kwa wanaume ilete mafanikio katika kupunguza maambukizi ya V.V.U., Mkoa unatarajia kutahiri jumla ya wanaume 264,990 ifikapo mwaka 2015”.

Wakati huohuo, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni tano kwa vituo vinne vya watoto yatima leo. Akitoa maelezo ya msaada huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Theresia Mahongo amesema kuwa Manispaa ya Iringa inao utaratibu wa kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima kulingana na majira na mahitaji. Miongoni mwa vitu vilivyotolewa kwa ajili ya watoto yatima ni pamoja na mchele, mafuta ya kupikia, maharage, unga, unga wa ngano, sabuni za kufulia na kuoga.
=30=