Sunday, October 7, 2012

MAONESHO YA ASALI DAR














SENJE AHIMIZA VIFUNGASHIO KATIKA BIDHAA





Halmashauri nchini zimeshauriwa kulipa kipaumbele suala la vifungashio katika mazao ya nyuki ili kutoa taarifa sahihi kwa mlaji.

Ushauri huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Immaculte Senje alipokuwa alitoa tathmini yake juu ya changamoto wanazokabiliana nazo katika kufikisha asali sokoni muda mfupi baada ya kutembelea mabanda ya Halmashauri katika maonesho ya kitaifa ya mazao ya nyuki yajulikanayo kama ‘Dar es Salaam Honey Exhibition’ yanayoendelea katika uwanja wa maonesho ya biashara ya Mwl. Julius Nyerere, barabara ya kilwa.

Senje amesema kuwa mabanda mengi aliyotembelea yanakabiliwa na changamoto ya vifungashio. Amesema “nadhani umefika wakati kwa Halmashauri zetu kulipa uzito suala la vifungashio katika mazao ya nyuki ili kuweza kuendana na uhalisia wa soko”. Amesema umuhimu wa vifungashio katika mazao ya nyuki hasa asali, unamuwezesha mlaji kupata taarifa kamili juu ya bidhaa anayoitumia na kiwango cha ubora wake.
Afisa Uhusiano wa Idara ya Uhamiaji Makao Makuu, Al-Haji M. Batenga alipotembelea banda la Manispaa ya Iringa katika Maonesho ya Asali

Mjasiliamali Msafiri Chengula kutoka kikundi cha Anamed chenye mizinga zaidi ya 200 katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa amesema kuwa changamoto wanayoipata ni uuzaji asali kwa njia ya lejaleja, jambo linalowasababishia tatizo katika kuhifadhi fedha na kuzipangia matumizi sababu fedha hizo hazikai. Amesema kuwa uchomaji misiti umekuwa ukiathili sana utengenezaji wa asali sababu nyuki wamekuwa wakikimbia au kuungua. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni tabia ya wizi wa asali katika kipindi cha uvunaji ambacho kwa wilaya ya Iringa amekitaja kuwa ni kati ya miezi ya Mei hadi Julai kutokana na ukame hali inayowalazimisha walinaji kuhamia msituni wakati huo.

Changamoto ya vifungashio pia linaikumba Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa mujibu wa Afisa Misitu wa Msaidizi, Enock Changime, amesema “sehemu ya kuhifadhia asili asali ili iweze kuingia sokoni kwa maana ya vifungashio ni tatizo kwa sababu vifungshio vingi vinatoka nchi ya Kenya”.

Changime amesema kuwa changomoto nyingine ni udogo wa mwamko wa jamii katika suala la ufugaji nyuki. Amesema manispaa ya Iringa imekuwa ikihamasisha  jamii kujiunga katika vikundi na kuvipa mafunzo juu ya ufugaji nyuki sambamba na na misaada ya mizinga ya kuanzia ufugaji huo. 

Amesema kutikana na changamoto ya uhaba wa wataalamu, Manispaa ya Iringa imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na sna na Halmashauri ya wilaya ya Iringa katika kuunganisha nguvu ya rasilimali wataalamu ili kuweza kukuza sekta ya nyuki katika halmashauri hizo.

Akiongelea umuhimu wa vifungashio katika kukuza soko la bidhaa nchini, Kaimu Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano kutoka Wakala wa Vipimo nchini Irene John amesema ili bidhaa iweze kutambulika ndani na nje ya nchi suala la vifungishio sahihi ni muhimu sana. Amesema kuwa ni vema kuyapa uzito unaoshahili mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa ufungashaji bidhaa za mazao ya nyuki, ameyataja mambo hayo kuwa ni masharti kuwa ni kuandika maelezo na kiasi cha ufungashaji. Mengine ameyataja kuwa ni uzuiaji wa ufungashaji wenye udanganyifu na uthibiti wa vipimo.

Maonesho ya kitaifa ya mazao ya nyuki yalianza katika uwanja wa maonesho ya biashara wa Mwl. Julius Nyerere tarehe 4-7 Oktoba, 2012 na yalitanguliwa na kongamano la kitaifa la wadau wa sekya ya asali kutokana na agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda.
=30=