Thursday, August 9, 2012

WILAYA ZATAKIWA KUJIFUNZA KILOLO


Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita ametoa wito kwa wilaya nyingine kuitembelea wilaya yake kwa lengo la kujifunza mikakati inayowawezesha kulima kwa ubora na uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa alipofanya mahojiano na gazeti hili katika banda la Wilaya ya Kilolo lililopo katika uwanja wa Maonesho wa John Mwakangale Uyole, Jijini Mbeya.

Guninita amesema kuwa wilaya yake imegawanyika katika ukanda wa juu unaohusisha tarafa ya Kilolo wenye miinuko na mabonde jambo linalofanya ugumu katika matumizi ya zana bora za kilimo kama powatila na matrekta.

Amesema ukanda wa chini wenye tarafa za Mazombe na Mahenge una maeneo ambayo ni tambarare pamoja na kuwa na ukame maeneo hayo yanafaa kwa matumizi ya zana bora za kilimo yakiwemo matrekta.

Guninita amesema pamoja na changamoto hiyo ya kijiografia na mabadiliko ya tabia nchi, bado wilaya yake inajivunia utaratibu wa wananchi wake wa kutunza mazingira hasa utunzaji wa vyanzo vya maji. Amesema utunzaji huu wa vyanzo vya maji una mchango mkubwa katika shughuli za kilimo jambo linalowawezesha wakulima wa wilaya hiyo kuweza kulima kwa mwaka mzima. Ameyataja mazao yanayolimwa zaidi kuwa ni maharage, njegere, mahindi, mbogamboga, magimbi, muhogo, na viazi mviringo.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo amesema kuwa wilaya yake imefanikiwa katika uhifadhi wa mazingira kwa uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine kuwekeza katika elimu ya uhifadhi wa mazingira. Amesema katika ziara zake za kutembelea wilaya yake baada ya uteuzi wake mapema mwaka huu, katika kata zote 22 alizotembelea amekuwa akisisitiza utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji. Aidha, wananchi wamehamasishwa kuacha vitendo vya uchomaji moto miti ya asili na misitu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mkakati mwingine ameutaja kuwa ni wananchi kuhamasishwa katika ulinzi shirikishi unaohusika katika kulinda misiti na hifadhi ya mazingira. Amesema “katika hili la uhifadhi wa mazingira baada ya kutoa elimu na hamasa wale wote watakaobainika watafikishwa katika mkondo wa sheria. Tumekuwa tukisisitiza sana Sheria ya Uhifadhi wa Mazingira ya mwaka 2004, inayotoa adhabu isiyopungua sh. 2,000,000, kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Akiongelea tuzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya utunzaji wa Mazingira kwa wilaya yake ya kilolo, Guninita amesema “katika kudhihirisha tabia ya uhifadhi wa mazingira kwa wilaya ya Kilolo, wilaya yetu imekuwa mshindi wa kwanza kitaifa. Kata ya bora ni Bomalang’ombe na taasisi bora imetoka katika wilaya yetu nayo ni gereza la Kihesa Mgagao”.

Amesema tuzo hiyo ya Rais, imeendelea kuamsha ari kwa wilaya yake, kuendelea kuhamasisha upandaji miti na uhifadhi wa mazingira. Ameitaja kampuni ya New Forest kuwa nayo inachangia kutoa hamasa kwa wananchi ya kupanda miti kwa wingi na kujiongezea kupato.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa katika kuhakikisha mkulima wa Kilolo anaendelea kuwa na lishe nzuri, wilaya yake imeendelea kuhamasisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Amesema katika kuhakikisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa unashika kasi, wananchi wamehamasishwa kuzitumia rasilimali walizonazo kufuga kisasa na ufugaji wenye tija. Amesema ufugaji wa kisasa na wenye tija ni ule wa ng’ombe wachache ambao mfugaji anaweza kuwahudumia vizuri na kuepuka mfugaji kuwa mtumwa kwa ngo’mbe wake.

Amesema Halmashauri yake kupitia DADPs imekuwa ikifanya vizuri katika hilo na ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma imeamsha ari zaidi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa wilayani hapo.
=30=

KILIMO HAI KIPEWE MSISITIZO ZAIDI



Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameshauriwa kutumia kilimo hai katika kujihakikishia uhai wa mazingira na usalama wa chakula kwa kukuza kipato na kupunguza gharama za uwekezaji katika kilimo.

Ushauri huo umetolewa na Lawrence Mgora, mkulima mwezeshaji wa kilimo hai kutoka taasisi ya uenezi wa elimu ya ugani na kilimo hai.

Akiongelea maana ya kilimo hai amesema kuwa ni kilimo kinachoangalia uhai wa mazingira, uhakika na usalama wa mlaji na usalama wa chakula jambo ambalo linamuhakikishia mkulima kipato kwa kutumia fursa alizonazo mkulima.

Mgora amesema kuwa ili kilimo kiwe kilimo hai ni lazima ulimaji wake ufuate kanuni za kilimo hicho. Amezitaja kanuni hizo kuwa ni pamoja na matumizi ya mbolea ya asili kama mchuzi wa mmea, uji wa mmea na lishe ya mmea katika uzalishaji wa mazao kwa kupandia na kukuzia. Kanuni nyingine amezitaja kuwa ni dawa za asili katika kudhibiti mmea shambani na katika hifadhi ya mazao pamoja na tiba asilia kwa mifugo wa aina yote. 

Akiongelea kwa mifano hai mafanikio ya kilimo hai kwa mkulima na jamii, Mkulima mwezeshaji huyo ameyataja kuwa ni kuongezeka kwa mapato kwa heka. Amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti walizofanya, mavuno ya mahindi yanayopatikana ni magunia 34 kwa heka kwa kutumia kanuni za kilimo hai ukilinganisha na magua 18 kwa kutumia kilimo cha kisasa. Ameongeza kuwa uzito wa mazao nao huongezeka, kwa debe la mahindi lililolimwa kwa kanuni za kilimo hai huwa na uzito wa kilo 22 ukilinganisha na kilo 18 kwa debe la mahindi lililolimwa kisasa. Akiongelea uhufadhi wa mazingira, amesema kuwa kilimo cha kisasa uharibu udongo jambo linalomlazimu mkulima kutumia mbolea mara kwa mara wakati kilimo hai kinahifadhi mazingira.

Akielezea nafasi ya ushirika katika kumsaidia mkulima wa Wilaya ya Kilolo, Afisa Uhirika Wilaya, Biezel Malia, amesema kuwa ushirika katika wilaya ya Kilolo umekuwa unalenga katika kumuwezesha mkulima kupata masoko ya mazao na mitaji kupitia Saccos na taasisi za kifedha. Amesema pia kupitia ushirika wilaya ya Kilolo imeweza kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa pembejeo za kilimo na zana za kilimo kama pawatila, matrekta.

Amesema pamoja na juhudi za wilaya kuwawezesha wakulima kupata mikopo kupitia Saccos na taasisi za kifedha, ipo changamoto ambayo wanachama wengi sio waaminifu katika kurejesha marejesho ya mikopo yao. Aidha, amesema kuwa changamoto nyingine ambayo wilaya yake inaifanyia kazi ni uhamasishaji juu ya umuhimu wa kuweka akiba ili kuweza kukopa baadae. Afisa Ushirika huyo amesema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ngazi ya wilaya, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 wilaya yake imetenga fedha za kutosha kutoa mafunzo ya kina kwa wakulima na wajasiliamali itakayoenda sambamba na elimu ya mikopo kwa wanachama wa Saccos.

Wilaya ya Kilolo ina aina nne ya vyama vya ushirika, vikiwepo vyama vya ushirika vya mazao (9), vyama vya akiba na mikopo (13), ushirika wa wapiga picha (1) na vyama vya wavuvi (2).
=30=

SERIKALI YABUNI MIKAKATI YA KUKUZA KILIMO



Serikali imeendelea kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbli ya kwa lengo la kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na chakula cha kutosha kwa wananchi wake na ziada kwa ajili ya watu wengine.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika kilele cha sikukuu ya wakulima na maonesho ya Nanenane mwaka 2012 yaliyofanyika kikanda katika viwanja vya Maonesho ya kilimo vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
 Mgeni rasmi katika kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dr. Christine Ishengoma alipotembelea banda ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa

Katika hotuba yake, Dkt. Christine amesema “katika jitihada za taifa letu za kujitosheleza kwa chakula, mikakati mbalimbali imeendelea kubuniwa na kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kanda ya Nyanda za Juu Kusini kupewa jukumu la kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi na kuwa ghala la chakula la Taifa kutokana na fursa nzuri za uzalishaji zilizopo hatika mikoa hii”.

Amesema ili jukumu hili la kitaifa lifanikiwe ni lazima wakulima wazalishaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutumia vizuri fursa zilizopo, kuzalisha kwa tija kwa kutumia kanuni bora za kilimo zitakazowawezesha kupata ziada ya chakula ya kuuza kwa mikoa mingine isiyokuwa na firsa nzuri za uzalishaji.

Akiongelea viwanzo tija vya uzalishaji wa mazao ya chakula, Dkt. Christine amesema “..viwango vya tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula kwa eneo bado viko chini. Takwimu zinaonesha kuwa, katika Nyanda za Juu Kusini uzalishaji wa mahindi kwa mfano, ni kati ya tani 2-3 kwa hekta moja wakati ambapo utafiti unaonesha kwamba hekta moja inaweza kuzalisha hadi tani 7”.Aidha, ametoa wito kwa viongozi na wakulima kuyatumia maonesho hayo kama jukwaa la kuwajengea uwezo wazalishaji wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuongeza tija na kufikia uwezo wa juu katika uzalishaji kadri inavyowezekana.

Akiongelea ufugaji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa kanda hiyo ina fursa ya ufugaji kutokana na uwepo wa ardhi, mvua za kutosha, miundombinu ya machinjio ya kisasa na rasilimali kubwa ya mifugo. Amesema mifugo imekuwa ikichangia katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa njia ya nguvu kazi na samadi. Amesema “katika kanda hii, asilimia 70 ya wakulima hutumia wanyamakazi katika shughuli za kilimo. Hii ni hatua kubwa inayostahili kupongezwa kwani matumizi ya nguvukazi ya wanyama ni moja kati ya teknolojia rahisi, sahihi na endelevu kwa wakulima wetu”.

Ikumbukwe kuwa sekta ya kilimo nchini inatoa ajira kwa karibia asilia 80. Vilevile, wakazi karibu asilimia 90 wa kanda ya Nyanda za Juu Kusini wanategemea kilimo kama shughuli kuu ya kiuchumi kwa mazao ya chakula na biashara.

=30=

MPAKA AWATAKA MPANDA KUPANDA MITI




 Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka ameshauri upandaji wa miti kwa wingi sana ili kuepukana na tatizo la wilaya hiyo kugeuka jangwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni katika kukausha zao la tumbaku linaloendelea kushamiri katika wilaya ya Mpanda mkoa mpya wa Katavi.

Ushauri huo ameutoa alipotembelea banda la wilaya ya Mpanda katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John Mwakangale- Uyole Mbeya.

Gertrude amesema kuwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni zinazotumika katika kukaushia zao la tumbaku, ni vizuri wilaya hiyo ikajipanga katika kupanda miti kwa wingi ili kuziba pengo la miti inayokatwa kwa ajili ya matumizi ya kuni katika kukaushia tumbaku. Amesema kuwa ni vema mkakati huo ukaanza mapema wakati njia mbadala ya nishati ya ukaushaji wa tumbaku ikiangaliwa ili kutokuteketeza misitu na mazao yake.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda 

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, amesema njia za kisayansi zinahitajika katika kukausha majani ya tumbaku pasipo kuharibu mazingira. Aidha, ametoa wito wananchi kufikiria njia ya kiteknolojia itakayotumika katika ukaushaji wa majani hayo. Amesema kwamujibu wa kaulimbiu ya maonesho ya Nanenane mwaka 2012 isemayo “Kilimo kwanza, zalisha kisayansi na kiteknolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu” vivyo hivyo wilaya ya Mpanda ifikirie hamasa ya maendeleo ya kiteknolojia katika kulifanya zao la tumbaku kuwa na tija zaidi katika ustawi wa wananchi na mazingira kwa ujumla wake.

Gertrude amesema kuwa ili kwenda sambamba na kauli mbiu hiyo, ni vizuri wilaya hiyo ikatoa hamasa zaidi katika utengenezaji wa zana zitakazosaidia katika kukipeleka mbele kilimo. Amesema kuwa wapo vijana wengi wanaoibuka na ubunifu wao kwa kutumia teknolojia rahisi wanaohitaji kupewa msukumo na kuendelezwa ili kuweza kuleta mapinduzi katika kilimo na ufugaji.

Akiongelea changamoto inayowakabili wanawake wajasiriamali katika upatikanaji wa masoko, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ametoa wito kwa wanawake wajasiriamali kuungama pamoja na kuunganisha nguvu zao katika shughuli zao za ujasiliamali. Amesema masoko ni changamoto inayowakabili wakina mama wengi wajasiriamali, na kushauri pindi wanapokuwa katika vikundi ni rahisi kwao kuweza kupatiwa mafunzo ya mbinu za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema umefika wakati kwa wanawake wa Nyanda za Juu kusini kuungana na kutumia fursa iliyopo sasa ya soko pana la Afrika ya Mashariki.
=30=