Katibu Tawala Mkoa wa Iringa,
Gertrude Mpaka ameshauri upandaji wa miti kwa wingi sana ili kuepukana na
tatizo la wilaya hiyo kugeuka jangwa kutokana na matumizi makubwa ya kuni
katika kukausha zao la tumbaku linaloendelea kushamiri katika wilaya ya Mpanda
mkoa mpya wa Katavi.
Ushauri huo ameutoa alipotembelea
banda la wilaya ya Mpanda katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John
Mwakangale- Uyole Mbeya.
Gertrude amesema kuwa kutokana na
matumizi makubwa ya kuni zinazotumika katika kukaushia zao la tumbaku, ni
vizuri wilaya hiyo ikajipanga katika kupanda miti kwa wingi ili kuziba pengo la
miti inayokatwa kwa ajili ya matumizi ya kuni katika kukaushia tumbaku. Amesema
kuwa ni vema mkakati huo ukaanza mapema wakati njia mbadala ya nishati ya
ukaushaji wa tumbaku ikiangaliwa ili kutokuteketeza misitu na mazao yake.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka alipotembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, amesema
njia za kisayansi zinahitajika katika kukausha majani ya tumbaku pasipo
kuharibu mazingira. Aidha, ametoa wito wananchi kufikiria njia ya kiteknolojia
itakayotumika katika ukaushaji wa majani hayo. Amesema kwamujibu wa kaulimbiu
ya maonesho ya Nanenane mwaka 2012 isemayo “Kilimo kwanza, zalisha kisayansi na
kiteknolojia kukidhi mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu” vivyo hivyo wilaya
ya Mpanda ifikirie hamasa ya maendeleo ya kiteknolojia katika kulifanya zao la
tumbaku kuwa na tija zaidi katika ustawi wa wananchi na mazingira kwa ujumla
wake.
Gertrude amesema kuwa ili kwenda
sambamba na kauli mbiu hiyo, ni vizuri wilaya hiyo ikatoa hamasa zaidi katika
utengenezaji wa zana zitakazosaidia katika kukipeleka mbele kilimo. Amesema
kuwa wapo vijana wengi wanaoibuka na ubunifu wao kwa kutumia teknolojia rahisi wanaohitaji
kupewa msukumo na kuendelezwa ili kuweza kuleta mapinduzi katika kilimo na
ufugaji.
Akiongelea changamoto inayowakabili wanawake wajasiriamali
katika upatikanaji wa masoko, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ametoa wito kwa
wanawake wajasiriamali kuungama pamoja na kuunganisha nguvu zao katika shughuli
zao za ujasiliamali. Amesema masoko ni changamoto inayowakabili wakina mama
wengi wajasiriamali, na kushauri pindi wanapokuwa katika vikundi ni rahisi kwao
kuweza kupatiwa mafunzo ya mbinu za upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya
nchi.
Amesema umefika wakati kwa wanawake wa Nyanda za Juu kusini
kuungana na kutumia fursa iliyopo sasa ya soko pana la Afrika ya Mashariki.
=30=
No comments:
Post a Comment