Sunday, August 5, 2012

WAKULIMA NA WASINDIKAJI WAWEZESHWE ASEMA RC IRINGA



Halmashauri za Wilaya na Manispaa zimeshauriwa kuwasaidia wakulima na wajasiliamali wasindikaji katika kuhakikisha bidhaa zao zinafikia viwango vya ubora vinavyotakiwa ili kujihakikishia soko la uhakika.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma alipotembelea mabanda ya wajasiliamali na wasindikaji katika maonesho ya Nanenane katika Uwanja wa John Mwakangale -Uyole Mbeya katika siku ya Iringa Day.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dr. christine Ishengoma (kulia) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi wa Fama Food Processing, Genovefa barnabas katika Uwanja wa Maonesho ya NaneNane Mbeya

Dkt. Christine amesema kuwa wakulima wasindikaji wanafanya kazi kubwa sana katika kusindika bidhaa za kilimo kwa kutumia juhudi zao wenyewe, hivyo kujikuta wakikwama katika utaalam na kushauri wawe wanapatiwa mafunzo na ushauri wa kitaalam ili kuufanya usindikaji wao uwe wa kisasa zaidi.

Amesema ni vizuri Halmashauri za Manispaa na Wilaya ziangalie jinsi ya kuwasaidia kitaalam na kiufundi ili bidhaa za usindikaji ziweze kufikia viwango vinavyokubalika na kupata lebo ya shirika la ubora (TBS). “watu wengi sasa wanaangalia lebo ya TBS ili kijihakikishia ubora hivyo ni vizuri mkahakikisha bidhaa zenu zinafikia ubora unaopkubalika na kupata lebo ya ubora” amesisitiza Dkt. Christine.

Akiongelea changamoto zinazowakabili wajasiliamali wasindikaji, mjasiliamali na mmiliki wa Fama Food Processing, Genovefa Barnabas amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wajasiliamali hasa wa Mkoa wa Iringa ni maeneo mahususi ya kuwawezesha kuzalishia bidhaa zao ili ziweze kupata uthibitisho wa ubora unmaotakiwa.  Akifafanua zaidi amesema “ili mjasiliamali anu wajasiliamali tuweze kutimiza ndoto zetu za kufanya shughuli za ujasiliamali vizuri ni vizuri serikali ikatusaidia kutenga maeneo ambayo yatakuwa mahususi kwa shughuli za ujasiliamali ambapo kila kitu kitakuwa kinafanyika hapo”. Amesema “kuanzia mazao na bidhaa zinapoletwa kutoka maeneo mbalimbali zinapokelewa katika eneo hilo, zinaanza kutengenezwa katika eneo hilo, zinapakiwa katika kontena, kufungwa na kuwekwa lebo hapohapo, kwa lugha nyingine mchakato wote unafanyika katika eneo moja hadi kwenda kwa mlaji”.

Akitetea umuhimu wa eneo hilo kwa wajasiliamali, Barnabas amesema kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa sababu kupatikana kwake kutawawezesha kupata cheti cha ubora wa bidhaa toka shirika la viwango (TBS). Amesema kitendo cha kupata lebo ya ubora toka TBS kutawafanya watu wengi zaidi kujiridhisha na ubora wa bidhaa hizo.  

Nunu Mtatifikolo ambaye ni Mwenyekiti kikundi cha Wanawake cha JAFAKU amesema changamoto ya watanzania kukubali bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wazalendo wa ndani ni mwiba katika ukuaji wao. “amesema ipo kasumba inayoendelea kutudidimiza ya wananchi kupenda bidhaa za nje tofauti na zinazozalishwa na wajasiliamali wa ndani”.

Amesema ili kuondokana na kasumba hiyo elimu inahitajika kutolewa kwa wananchi ili waweze kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. “Elimu hiyo itasaidia sana kubadili kasumba hii na elimu hii inatakiwa kuambatana na matangazo ya bidhaa za wajasiliamali” amesisitiza Mtatifikolo.

Mwenyekiti wa kikundi cha Wanawake wa KKKT-Nduli, Laurencia Malila amesema katika banda la Manispaa ya Iringa amesema kuwa wanawake wajasiliamali Mkoani Iringa wanakabiliwa na changamoto ya masoko kwa maana ya wanunuzi wa bidhaa zao. Amesema “pamoja na kuwa na bidhaa nzuri bado wananchi wanamuitikio mdogo wa kuzinunua jambo linalowafanya washindwe kuzalisha bidhaa kwa wingi”.  

Malila ambaye pia kikundi chake kinajihusisha na kilimo cha kisasa na ufugaji wa nyuki kikiwa na mizinga 47 ya nyuki ya kisasa, ametoa wito kwa watu wanaopenda kujifunza kilimo cha kisasa cha mahindi na maharage pamoja na ufugaji wa nyuki kuwatenbelea ili kujifunza katika mashamba darasa yao yaliyopo katika kata ya Nduli.

=30=

No comments:

Post a Comment