Zana ya Kilimo Kwanza itafanikiwa kwa wakazi wa kanda ya Nyanda
za Juu Kusini kulima kilimo cha kisayansi na kiteknolojia zaidi na kukifanya
kilimo kiwe cha kibiashara.
Ushauri huo umetolewa katika majumuisho baada ya mgeni rasmi Dkt.
Christine Ishengoma kutembelea mabanda ya maonesho ya Nanenane kanda ya nyanda
za Juu Kusini katika siku ya mkoa wa Iringa (Iringa Day) iliyofanyika katika
uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John Mwakangale Uyole Mbeya.
Dkt. Chrisrine ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema
“kimsingi kilimo kwanza ni Nyanda za Juu Kusini yaani Mikoa ya Iringa, Njombe,
Ruvuma, Mbeya, Rukwa na Katavi kwa kuwa mikoa hii ndio wazalishaji wakubwa
nchini, hivyo huwezi kutenganisha Kilimo Kwanza na Nyanda za Juu Kusini”. Amesema katika kuendeleza kilimo katika ukanda
huo ni lazima kilimo kiwe cha kisayansi na kiteknolojia zaidi ili kuwawezesha
wakulima kulima maeneo madogo lakini kwa kupata mazao mengi zaidi na yenye
ubora unaotakiwa. Amesema kuwa wakulima wameendelea kupata hasara katika kilimo
kwa kutokufuata kanuni za kilimo bora jambo linalowafanya waweke nguvu nyingi
katika kilimo lakini matokeo wanayoyapata hayaendani na nguvi halisi
waliyowekeza katika kilimo hicho. Aidha, ametoa wito kwa wataalam wa kilimo
kuwa karibu zaidi na wakulima ili kuwafundisha waweze kuepukana na kilimo cha
kizamani na kimazoea.
Hapa huitaji maelezo zaidi ya picha kujieleza yenyewe
Akiongelea kuhama kutoka katika kilimo kidogo kwa ajili ya
kujitosheleza kwa chakula, amesema “umefika wakati sasa wa kuhama kutoka katika
kilimo cha kawaida na kukifanya kilimo chetu kiwe cha kibiashara. “Na hili
litawezekana pale tu tutakapokifanya kilimo chetu kuwa kilimo cha kisayansi
zaidi” amesema Dkt. Christine.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amesema baada ya kutembelea
mabanda ya maonesho mikoa yote inafanya vizuri. Amesisitiza kuwa ili maonesho
hayo yawe mazuri zaidi ni vema maandalizi yake yakaanza mapema zaidi katika
Halmashauri zote.
Akielezea nini amejifunza katika maonesho hayo, amesema kuwa
amejifunza mambo mengi sana ambayo baadhi hakuwa akiyafahamu kabisa, baadhi
amejikumbusha baada ya kupita muda mrefu tokea ayafahamu na kusema “maonesho
yaha yamekuwa ni shamba darasa kwa watu wengi”. Baada ya kujionea ubunifu wa
kiteknolojia kutoka kwa wananchi mbalimbali, ametoa wito kwa mikoa hiyo ya
nyanda za juu kusini kuwaangalia wabunifu hao kwa jicho la pekee ili waweze
kuwaendeleza zaidi na wao kunufaika na ubunifu wao. Amesema kuwa imani yake ni
kwamba pale juhudi za pamoja zitakapowekwa hakika kilimo kitatoka katika hali
yake ya sasa na kuwa bora zaidi.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameweka rekodi katika
maonesho hayo ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda 40 ya maonesho kwa siku
na kupokea maelezo na kuuliza baadhi ya maswali kwa waoneshaji mbalimbali.
=30=
No comments:
Post a Comment