Thursday, September 9, 2010

Maziwa ya mama hujenga mahusiano kati ya mama na mwana

Maziwa ya mama ndiyo chakula pekee na cha asili kinachompa mtoto afya na nguvu na kinasaidia kujenga uhusiano mwema baina ya mamam na mtoto imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Aida Kapwani wakati akiwafundisha akina mama waliohudhuria kliniki ya watoto wachanga mada ya afya ya mama na mtoto katika hospitali ya mkoa wa Iringa leo.

Kapwani amesema “kitendo cha mama kunyonyesha mtoto wake maziwa ya mama kinamfanya mtoto awe na afya njema na nguvu sababu maziwa ya mama ni chakula kamili na cha asili kwa mtoto mchanga”. Ameongeza kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama unamjenga mtoto kisaikolojia na kuuisha uhusiano baina ya mama na mtoto.

Kapwani amesisitiza kuwa pasina sababu yoyote au maelekezo yoyote toka kwa daktari ni lazima mtoto anyonye maziwa ya mama pekee kwa kipindi chote cha miezi sita mfululizo bila kuchanganya na kitu chochote. Amesema “maziwa ya mama ni chakula kamili na kinywaji cha kwanza kwa mtoto mchanga”.

Akielezea faida za maziwa ya mama kwa mtoto mchanga, Kapwani amesema kuwa yanamuondolea mtoto hatari ya kushambuliwa na magonjwa kama vile utapiamlo, kuhara, kutapika na kudumaa. Faida nyingine ameitaja kuwa ni mtoto kupata virutubisho vyote stahili vya mwilini. Aidha ameongeza kuwa faida nyingine ya mama kunyonyesha mtoto maziwa ya mama kunamuwezesha mama kutopata upungufu wa damu na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Katika darasa la kliniki hiyo lililohudhuriwa na akina mama zaidi ya hamsini, Kapwani alikatishwa taa na ushiriki na muitikio wa akina baba katika elimu ya afya ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kliniki. Aidha alichukua fursa hiyo kuwapongeza akina baba wawili aliohudhuria darasa la klini hiyo na kutoa wito kwa akina baba wote kuwasindikiza wake zao pindi wanapoenda klinini na kupatiwa mafunzo ya afya ya uzazi wa mama na mtoto.

Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa ambayo akina baba wanamuitikio hafifu sana wa kuhudhuria kliniki ya afya ya uzazi wa mama na mtoto.


Picha ya mtoto akitumia haki yake hotelini