Wednesday, August 3, 2016

JAMII YATAKIWA KULA VIAZI LISHE KUEPUKA UTAPIAMLO



Na Mwandishi Maalum Mbeya

Jamii imehimizwa kutumia viazi lishe vyenye virutubishi kwa lengo la kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa mama wajawazito na watoto.

Akielezea umuhimu wa viazi lishe vyenye virutubishi katika kukabiliana na tatizo la lishe Mkoani Iringa, Afisa kilimo, umwagiliaji na ushirika, Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu alisema kuwa kutokana na Mkoa wa Iringa kuwa na tatizo la utapiamlo kwa kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. 

Alisema kuwa viazi lishe vyenye virutubishi vina rangi ya karoti na wingi wa vitamin A ya kibaolojia inayohitajika kwa kina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Alisema kuwa Halmashauri hiyo imeandaa mashamba ya mbegu kwa lengo la kuzalisha mbegu za kutosha ili wananchi wazipate kwa urahisi.

Akiongelea faida zake, alizitaja kuwa ni majani ya viazi vitamu yana vitamin A na B,madini ya chuma na protini kwa wingi. Faida nyingine vinaweza kutumika kama chakula cha mifugo. Aliongeza kuwa aina mpya ya viazi lishe inaweza kuota popote ha kutoa mazao kwa wingi na vinaweza kuchanganywa na mazao mengine. Pamoja na kutumika kwa chakula, viazi lishe pia vinatumika kutengeneza chapati, maandazi, uji na sharubati.  

Halmashauri ya wilaya ya Iringa kwa kushirikiana na mradi wa Vista kutoka nchini Marakani uliotoa mbegu katika vijiji 36 vya Wilaya ya Iringa ambavyo tayari vinazalisha viazi lishe.

=30=

JAMII IMETAKIWA KUTUMIA CHUMVI YENYE MADINI JOTO KUEPUKA ULEMAVU



Na Mwandishi Maalum Mbeya

Jamii imetakiwa kutumia chumvi yenye madini joto ili kujenga ukuaji wa akili na kuepukana na ulemavu.

Kauli hiyo litolewa na Afisa Lishe Manispaa ya Iringa, Anzael Msigwa alipokuwa akifafanua umuhimu wa madini ya joto katika chumvi ya majumbani kwa wananchi waliotembelea banda la maonesho la Manispaa ya Iringa lililopo katika uwanja wa John Mwakangale jijini Mbeya.

Msigwa alisema “madini joto ni madini ambayo yanawekwa kwenye chumvi ili kuzuia ugonjwa wa tezi la shingo na kwa mama wajawazito madini hayo yanazuia baadhi ya ulemavu wa viungo kwa watoto. Madini joto yanasaidia ubongo wa mtoto akiwa tumboni kukua vizuri na kuzuia udumavu”.

Akiongelea umuhimu wa madini joto mwilini, Msigwa alisema kuwa madini joto yanahitajika kwa wingi wakati wa mabadiliko ya kimwili hasa kuvunja ungo, kubalehe na wakati wa ujauzito. Faida nyingine ya madini hayo ni kusaidia ukuaji wa mtoto aliye tumboni na ukuaji wa maendeleo yake baada ya kuzaliwa. Madini hayo pia husaidia ukuaji wa mwili na akili.

Afisa lishe huyo alisema kuwa kukosekana kwa madini joto mwilini, husababisha uvimbe wa tezi la shingo, ugumu katika kuelewa na kufundishika na kudumaa mwili na utaahira. Athari nyingine ni kuharibika kwa mimba na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu na mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo.

Alishauri kuwa chumvi inatakiwa kuhifadhiwa katika kasha kavu, lenye mfuniko na kuhifadhiwa mbali na joto.

Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya chumvi ya mwaka 2010, inatoa idhini kwa maafisa wenye dhamana kukagua chumvi sehemu za kuhifadhi na kuuza chumvi.

=30=




NTINIKA ALITAKA JIJI MBEYA KUJIKITA KATIKA USAFI



Na Mwandishi Maalum Mbeya 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika amelitaka jiji la Mbeya kujikita katika kudhibiti taka ili liwe jiji la mfano nchini kwa kuwahakikishia wakazi wake afya njema na usafi wa mazingira ili kuepukana na magonjwa.

Kauli hiyo aliitoa baada ya kufanya ziara ya kukagua hali ya usafi katika baadhi ya madampo ya taka jijini Mbeya leo asubuhi.

Katika ziara hiyo Ntinika aliyeambatana na Afisa Afya wa Jiji hilo na mjumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya ya Mbeya alibaini uchafu uliotakapaa katika madampo ya taka katika shule za msingi za Manga, Sinde na Mbata zilizopo katikati ya jiji hilo. Katika maeneo yote hayo yaliyotembelewa makasha ya kuhifadhia taka yalikuwa yamejaa huku uchafu mwingine ulikuwa umetakapaa chini. Alimtaka Afisa Afya wa jiji hilo kuhakikisha uchafu huo unazolewa na kupelekwa katika dampo kubwa kwa ajili ya kuhifadhiwa ili wananchi waweze kutekeleza majukumu yao.

Ntinika alisema kuwa anataka jiji la Mbeya liwe la mfano katika usafi ili majiji mengine wajifunze kutoka hapo. Alisema usafi ni agenda yake ya mbele kwa sababu usafi utawafanya wananchi wa jiji hilo kuwa na afya njema na uhakika wa maisha marefu na kuepukana na magonjwa ya mlipuko.

Katika shule ya msingi Sinde iliyopo Kata ya Sinde jijini hapa, Semeni Kemendu, mwanafunzi wa darasa la saba alisema kuwa hali ya usafi katika dampo lililopo shuleni hapo imekuwa mbaya kwa kipindi kirefu. Alisema kuwa pembeni mwa dampo hilo kuna kina mama ntilie wanaopika chakula katika mazingira hayo machafu. Aliongeza kuwa kutokana na hali ya uchafu masomo kwa baadhi ya wanafunzi yamekuwa ya kusuasua. 

Mara nyingi wanafunzi huumwa tumbo na kulazimika kuomba ruhusa mara kwa mara” alisema Kemendu.

=30=

NTINIKA ATAKA ACB KUJITANGAZA



Na Mwandishi Maalum Mbeya 

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ameitaka benki ya kibiashara ya Akiba (Akiba Commercial Bank) kujitangaza zaidi katika vyombo vya habari ili iweze kufahamika zaidi kwa wananchi.

Ushauri huyo aliutoa alipotembelea benki hiyo katika viwanja vya John Mwakangale katika maonesho ya Nanenane jijini Mbeya.

Ntinika alisema kuwa ili benki hiyo na huduma zake ziweze kufahamika zaidi kwa wananchi lazima benki hiyo itengeneze mkakati wa kujitangaza kwa wananchi kupitia vyombo vya habari. “Pamoja na huduma nzuri mnazozitoa lakini kama hamjitangazi si rahisi kwa wananchi kuwafahamu na kufahamu huduma zenu. Tumieni fursa hii ya maonesho ya kilimo Nanenane kujitanga zaidi na hasa kutangaza mipango yenu ya kumnufaisha mkulima pamoja na mambo mengine” alisema Ntinika.

Ntinika ambaye pia ni mtaalam mbobezi katika masuala ya fedha na ukaguzi wa mahesabu, alisema kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya kibenki hivyo kukosa huduma na fursa nyingi zinazopatikana kupitia taasisi za kifedha. Aliitaka benki hiyo kupanua wigo wake wa huduma ili kuwanufaisha wananchi wengi wa wilaya ya Mbeya.

Nae Afisa mikopo wa benki ya kibiashara ya Akiba, Anthony Kunambi alisema kuwa benki yake inalenga wajasiliamali wadogo na wa kati kwa kuwapa elimu ya ujasiliamali ili waweze kufanya kazi zao kwa tija na faida zaidi. Alisema kuwa miongoni mwa huduma wanazotoa ni pamoja na akaunti za amana, hundi, akaunti maalumu ya wafanyabiashara na huduma za kuwaleta karibu Vicoba na taasisi za kifedha na kuwaelimisha umuhimu wa Vicoba kutumia huduma za kibenki badala ya mfumo wa awali wa kujiwekea akiba majumbani.

Akiongelea jinsi benki yake inavyojishughulisha na kilimo, Kunambi alisema kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa huduma ya mikopo kwa wakulima na wafugaji. 

Kwa mkoa wa Mbeya tumekuwa tukitoa mikopo kwa wafugaji wanaofuga kisasa lakini katika mkoa wa Arusha tumekuwa tukifanya kazi na wafugaji wanaofuga kizamani. Katika mkoa wa Arusha tumekuwa tukifadhili mradi wa kunenepesha ng’ombe na wanyama wamekuwa wakikatiwa bima ili kumhakikishia mfugaji uhakika kwa mifugo yake endapo janga litatokea”.

Sabina Stanley ambaye ni msimamizi wa mikopo wa benki hiyo tawi la Mbeya, alisema kuwa benki hiyo imaendelea na mradi wa majaribio katika sekta ya kilimo kwa kuanza na miradi michache katika mikoa ya Mbeya, Arusha na Dodoma. Alisema kuwa benki yake ilitoa mikopo kwa wakulima wa Litenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa vikundi 39 vya wakulima mwaka 2015. Nyingine ni mashine ya kukaushia kahawa yenye thamani ya dola za mimarekani 200 na kampuni ya Rogimwa iliyokopeshwa milioni 200.

Benki ya kibiashara ya Akiba (ACB) ina jumla ya matawi 18 kati ya matawi hayo, 13 yapo mkoani Dar es Salaam, wakati mikoa ya Mbeya, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma ikiwa na tawi mojamoja.
=30=


WATEJA WA MAMLAKA YA MAJI MBEYA MJINI WATAKIWA KUWA WALINZI WA MIUNDOMBINU YA MAJI MBEYA



Na Mwandishi Maalum Mbeya

Wateja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Mbeya wametakiwa kuwa walinzi wa miundombinu ya maji ili idumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa huduma kwa wateja wa Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Mbeya, Hilda Nzary alipokuwa akielezea umuhimu wa mkataba wa huduma kwa mteja wa mamlaka hiyo katika viwanja vya Nanenane jijini Mbeya.
Afisa Huduma kwa Wateja, Hilda Nzary

Nzary alisema “kwa mujibu wa mkataba wa huduma kwa mteja, wajibu wa mteja ni kuzuia wizi, uharibifu mchepusho wa mita na vitendo vya rushwa ikiwa watumishi wa mamlaka wameomba”

Aliongeza kuwa mteja anawajibu wa kutoa taarifa kwa uongozi wa mamlaka juu ya vitendo vyovyote vinavyohatarisha usafi na usalama wa maji ili huduma hiyo iendelee kuwa salama kwa jamii nzima na kuwa endelevu. Mteja pia anawajibu wa kulipia huduma ya majisafi na majitaka na kutunza dira ya maji inayopima wingi wa maji yanayotumika.

Afisa huduma kwa wateja alisema kuwa, kwa wateja kutimiza wajibu huo, watarajie huduma bora ya uhakika na yenye ufanisi wa hali ya juu katika muda mfupi na kurejeshewa huduma ya maji katika muda usiozidi saa 24 baada ya kulipia ankara yake yote. Aliongeza kuwa mteja anayo haki ya kutoa taarifa kwa maandishi iwapo haridhiki na huduma anazopata.

Akiongelea ubora wa huduma zitolewazo na mamlaka hiyo, alisema kuwa mamlaka hiyo itahakikisha inaendelea kuimarisha viwango vya ubora wa huduma zinazotolewa kwa kupitia hali ya utendaji kila baada ya miezi mitatu. Mamlaka imeweka mtandao wa kukusanya habari kutoka kwa wateja wa ndani na wateja wa nje ili iweze kupata taarifa sahihi zitakazoisaidia kufanya maamuzi sahihi ya kuboresha huduma kwa wateja.

Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira mjini Mbeya ilianzishwa mwaka 1998 kwa Sheria namba 8 ya Maji, ya mwaka 1997 kifungu 3(1) ikiwa inahudumia wateja 48,000.
=30=