Na Mwandishi Maalum Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika
amelitaka jiji la Mbeya kujikita katika kudhibiti taka ili liwe jiji la mfano
nchini kwa kuwahakikishia wakazi wake afya njema na usafi wa mazingira ili
kuepukana na magonjwa.
Kauli hiyo aliitoa baada ya kufanya
ziara ya kukagua hali ya usafi katika baadhi ya madampo ya taka jijini Mbeya
leo asubuhi.
Katika ziara hiyo Ntinika aliyeambatana
na Afisa Afya wa Jiji hilo na mjumbe wa kamati ya usalama ya Wilaya ya Mbeya alibaini
uchafu uliotakapaa katika madampo ya taka katika shule za msingi za Manga,
Sinde na Mbata zilizopo katikati ya jiji hilo. Katika maeneo yote hayo
yaliyotembelewa makasha ya kuhifadhia taka yalikuwa yamejaa huku uchafu mwingine
ulikuwa umetakapaa chini. Alimtaka Afisa Afya wa jiji hilo kuhakikisha uchafu
huo unazolewa na kupelekwa katika dampo kubwa kwa ajili ya kuhifadhiwa ili
wananchi waweze kutekeleza majukumu yao.
Ntinika alisema kuwa anataka jiji la
Mbeya liwe la mfano katika usafi ili majiji mengine wajifunze kutoka hapo.
Alisema usafi ni agenda yake ya mbele kwa sababu usafi utawafanya wananchi wa
jiji hilo kuwa na afya njema na uhakika wa maisha marefu na kuepukana na
magonjwa ya mlipuko.
Katika shule ya msingi Sinde iliyopo
Kata ya Sinde jijini hapa, Semeni Kemendu, mwanafunzi wa darasa la saba alisema
kuwa hali ya usafi katika dampo lililopo shuleni hapo imekuwa mbaya kwa kipindi
kirefu. Alisema kuwa pembeni mwa dampo hilo kuna kina mama ntilie wanaopika
chakula katika mazingira hayo machafu. Aliongeza kuwa kutokana na hali ya
uchafu masomo kwa baadhi ya wanafunzi yamekuwa ya kusuasua.
“Mara nyingi wanafunzi huumwa tumbo na
kulazimika kuomba ruhusa mara kwa mara” alisema Kemendu.
=30=
No comments:
Post a Comment