HIFADHI ZA TAIFA
TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
Kisiwa cha Saanane kimetangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa
kufuatia Tangazo la Serikali Namba 227 lililotolewa hivi karibuni.
Kutangazwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane kunafuatia
kupitishwa kwa Azimio la Bunge mwezi Oktoba mwaka jana lililoridhia kupandishwa
hadhi kwa kisiwa hicho kutoka Pori la Akiba na kuwa Hifadhi ya Taifa.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane itakuwa na ukubwa wa
kilomita za mraba 2.18 na itajumuisha maeneo ya lililokuwa Pori la Akiba ,
Visiwa vya Chankende kubwa na ndogo pamoja na eneo la maji ya Ziwa Victoria
linalozunguka visiwa hivyo.
Kuanzishwa kwa Hifadhi mpya ya Taifa ya Saanane kutawezesha haja
ya kuongeza spishi mbalimbali za wanyamapori na hivyo kuongeza utalii wa mjini,
utalii wa ndani, utafiti na kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi na wananchi
watakaotembelea hifadhi hii mpya.
Aidha, uamuzi huu utasaidia kutunza hali ya bioanuwai, uhifadhi
wa mazalia na makuzio ya samaki na uendelezaji wa utalii wa mjini kuendelea
kuimarika.
Kabla ya kupandishwa hadhi, Kisiwa cha Saanane kilikuwa Bustani
ya wanyama mwaka 1964 kabla ya kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1991.
Ilipofika mwaka 2006, Serikali ilikikabidhi kisiwa hicho kwa Shirika la Hifadhi
za Taifa kwa ajili ya kukiendesha na kusimamia mchakato wa kukipandisha hadhi
kuwa Hifadhi ya Taifa.
Kufuatia
uamuzi huu, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) sasa litakuwa na jumla ya
Hifadhi 16 nchi nzima ambazo nyingine ni pamoja na Serengeti; Ziwa Manyara;
Tarangire na Arusha.
Nyingine
ni pamoja na Kilimanjaro; Mkomazi; Saadani; Mikumi; Milima ya Udzungwa; Ruaha;
Kitulo; Katavi; Gombe; Milima ya Mahale na Kisiwa cha Rubondo.
Wakati
huohuo,
eneo la Hifadhi ya Taifa Gombe limeongezwa ukubwa kutoka Kilometa za mraba
33.74 hadi kufikia kilometa za mraba 56. Uamuzi huu unatokana na Tangazo la
Serikali Namba 228 lililotolewa hivi karibuni ambalo linafuatia Azimio la Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililotolewa mwaka jana linalohusu
kuridhiwa kwa uamuzi wa kurekebisha mipaka ya Hifadhi ya Taifa Gombe kwa
kuondoa eneo la makaburi na kuliacha kwa wananchi pamoja na kujumuisha eneo la
ufukwe wa maji ya Ziwa Victoria na eneo la ukanda wa maji.
Kuongezeka
kwa eneo la ufukwe wa ziwa na ukanda wa maji kwenye eneo la hifadhi kutaongeza
wigo wa shughuli za utalii katika Hifadhi kama vile kuogelea, utalii wa boti,
mitumbwi na uvuvi wa kitalii.
Imetolewa na Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S. L. P 3134
ARUSHA