Na.
Bruno Machary, IRINGA
Serikali Mkoani Iringa imejipanga kutekeleza kwa vitendo utaratibu
wa matokeo makubwa sasa (BRN) ili kufikia malengo yaliyowekwa kitaifa ya kutoa
huduma bora kwa wananchi.
Hayo yamejidhihirisha jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Dkt. Christine
Ishengoma kufanya ziara katika Halimashauri za Mkoa wa Iringa kwa lengo la
kuhamasisha utendaji wa kazi kwa wafanyakazi wa kada mbalimbali kupitia
utaratibu wa matokeo makubwa sasa. Katika ziara hizo pamoja na mambo mengine
amekuwa akisikiliza changamoto na kero na kuzipatia ufumbuzi.
Akiongea na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa
katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Dkt. Ishengoma amesema kuwa wataalamu hawapaswi kukaa ofisini tu ila wanapaswa
kutoka na kuwasikiliza wananchi ili kutatua kero zinazowakabiri kwa urahisi.
Amesema kuwa wataalamu hao ndio suluhisho la kero hizo zinazowakabili wananchi
katika kufikia maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii. Amesema kuwa kila
mfanyakazi analo jukumu la kujitazama na kujihoji yeye wenyewe jitihada alizofanya
katika kufikia malengo ya Serikali.
“Utendaji kazi ubadilike na kila mmoja aipende kazi yake
kulingana na kada aliyonayo” amesema Dkt. Ishengoma.
Akiongelea dhana ya mawasiliano katika kuleta ufanisi wa kazi,
Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mawasiliano ni jambo la muhimu sana kwa wafanyakazi kwasababu
yanasaidia kuleta ushirikiano na upendo miongoni mwa wafanyakazi hatimae
kuondoa chuki baina yao. Amesema kuwa mawasiliano yanapokuwa mazuri ufanisi wa
kazi unakuwa mzuri pia.
Amewashauri wafanyakazi kuwashirikisha wakuu wa idara zao pale
wanapokabiliwa na matatizo mbalimbali katika utendaji kazi wao. Amesema kuwa ni
vizuri kutatua matatizo yanayojitokeza kupitia vikao rasmi vya idara kabla ya
kuyawasilisha ngazi za juu.
Matokeo makubwa sasa (B.R.N) ni utaratibu wa utendaji kazi
ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kutoa ufanisi wa kazi unaopimika haraka.
Maeneo ya kipaumbele katika BRN ni elimu, nishati, maji, uchukuzi, mapato na
kilimo.
=30=
No comments:
Post a Comment