Na. Bruno Machary, IRINGA
Serikali Mkoani Iringa imejidhatiti
kufanikisha mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi unafanyika pasipo kuwepo na vitendo
vya udanyanyifu.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Mwl.
Joseph Mnyikambi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliomtembelea ofisini
kwake ili kujua jitihada zilizochukuliwa na Mkoa katika kukabiliana na vitendo vya
udanganyifu kwa walimu na wanafunzi wakati wa mtihani huo.
Akitoa ufafanuzi, Mnyikambi amesema kuwa wamejitahidi kutoa semina
kwa walimu ili kuhakikisha kuwa mtihani huo
unafanyika kwa haki na amani pasipo kuwepo kwa vitendo vyovyote vya udanganyifu
kwa wanafunzi wala walimu watakaosimamia mtihani huo. Kwa upande wa wanafunzi,
amesema kuwa kila mwanafunzi atatumia dawati lake ili kuondoa mianya inayoweza
kushawishi udanganyifu.
Akiongelea upande wa maandalizi ya mtihani huo, amesema kuwa maandalizi
yote yamekamilika na vifaa vyote vimeshafika
Mkoani na vimeshapelekwa kila Halmashauri. “Vifaa vyote vinavyohusu masuala ya mtihani
huo vimeshafika Mkoani hapa na vimeshapelekwa katika wilaya zote” amesema
Mnyikambi.
Afisa Elimu huyo amesema kuwa katika mwaka wa masomo 2013 idadi ya wanafunzi wanaotarajiwa kufanya
mtihani huo imepungua kwa jumla ya wanafunzi 1194 ikilinganishwa na mwaka wa
masomo 2012. Kwa mwaka 2012 kulikuwa na watahiniwa 24,342 wakati mwaka huu wapo
watahiniwa 23,148.
Mtihani huo unaotarajiwa kuanza kufanyika siku ya jumatano ya tarehe
11/9/2013 kitaifa, utajumuisha shule za msingi 466 za Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa una jumla ya
wilaya tatu ambazo ni Iringa, Mufindi na Kilolo, zenye jumla ya Halmashauri
nne.
=30=
No comments:
Post a Comment