Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu
ilipokabidhi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.
Leodegar Tenga, Rais wa TFF
Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi
kwa lengo la kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo
ambalo limeleta mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa
marefa na makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa
moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani
tumeanzisha jambo hili kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema
Rais Tenga wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali
vya habari.
Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na
utawala bora watu wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni
lazima kwa kampuni kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.
Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola
katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania
ndiyo yenye udhamini mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo
ya televisheni.
Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu
za Ligi Kuu hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti
zao za mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika
zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga
amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na
liko katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza
haraka iwezekanavyo.
“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa
sababu ambazo haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu
katika karibu viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer
(mashine za kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa
Taifa, system (mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa
tunaangalia uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa
Taifa una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala
lisitucheleweshe,” amesema.
=30=
No comments:
Post a Comment