Friday, October 1, 2010

Mparaganyiko wa kijamii chanzo cha watoto wanaoishi katika mazingira magunu 

Matokeo ya umasikini, mparaganyiko wa kijamii na madhara ya ugonjwa wa ukimwi ndiyo vichochezi vikubwa vya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi katika miaka ya hivi karibuni imefahamishwa.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, mama Gertrude Mpaka wakati akifungua warsha ya siku tano ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu iliyofanyika katika hoteli ya Wilolesi Hill Top katika Manispaa ya Iringa.

Katibu Tawala Mkoa akisoma hotuba yake

Mama Mpaka amesema mazingira haya ya umasikini na mparaganyiko wa kijamii unawaathiri kwa kiwango kikubwa watoto kuweza kupata haki zao za msingi kama vile uangalizi wa karibu, msaada na kulindwa. Aidha ameongeza kuwa mazingira hayo yamechangiwa pia na utaratibu wa asilia wa familia na jamii kuweza kuwachukua baadhi ya watoto na kuwalea unaendelea kutoweka kutokana na sababu za kijamii na kiuchumi kama umasikini uliokithiri na ugonjwa wa ukimwi. 

Kutokana na kadhia hiyo Katibu Tawala Mkoa ameyataja makundi yanayoathirika zaidi ni wanawake, vijana, na watoto kwa umasikini pamoja na sababu nyingine. Mathila hayona ukubwa wa tatizo unajidhihirisha katika familia, jamii na sekta mbalimbali katika mkoa wa Iringa. Amesema kuwa watu wengi wanapoteza maisha na kuacha idadi kubwa ya yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Aidha mkoa wa Iringa unakadiriwa kuwa na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wapatao 67,998, miongoni mwao wasichana ni 35,068 na wavulana ni 32,930. Kati yao asilimia 29 ni yatima.

Mama Mpaka amesema kutokana na tatizo la umasikini katika mkoa wa iringa changamoto iliyopo ni uwezo wa kutoa huduma stahili kwa watoto zitakazoweza kuboresha maisha yao. Amesema kuwa watoto wanahitaji afya, elimu, makazi, usalama, chakula na msaada wa kisaikolojia kwa ajili ya ustawi wao.

Warsha hiyo ya siku tano imeandaliwa na shirika la ESRF kwa kushirikiana na UNICEF na imewahusisha maafisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri, mkoa na wadau mbalimbali.