Katibu Tawala
Mkoa wa Iringa, Getrude K. Mpaka ameishauri Wizara ya Fedha kuangalia uwezekano
wa kuongeza wigo wa fedha katika bajeti za Mikoa ili kuweza kuiwezesha mikoa
kushiriki kikamilifu katika michezo ya shirikisho la michezo kwa Wizara na Idara
za Serikli (SHIMIWI).
Ushauri huo
ameutoa katika hafla fupi ya kukabidhiwa kikombe na kuipongeza timu ya kuvuta
kamba wanawake ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa baada ya kuibuka mshindi wa
pili nyuma ya timu ya Ikulu kwa mchezo wa kuvuta kamba wanawake kutoka klabu ya
Ras Iringa iliyoshiriki katika mashindano hayo mjini Morogoro.
Nahodha wa timu Agnes Mlula (kulia) akimkabidhi kombe
mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka
Mpaka amesema “ni
vizuri Wizara ya Fedha iangalie jinsi ya kuongeza ceiling kwa Mikoa ili
watumishi wetu waweze kushiriki kikamilifu kama
watumishi wa timu za Wizara na kutokujiona ni wanyonge”. Amesema kuwa mwakani
Ofisi yake itajipanga vizuri zaidi ili iweze kupeleka timu kubwa zaidi ya
wachezaji wengi katika michezo tofauti tofauti.
Ameitaka timu
hiyo kutobweteka na kuendelea na mazoezi makali ili mwakani iweze kuibuka
mshindi wa kwanza. Katika kufanikisha hilo
amemuagiza Afisa Michezo Mkoa wa Iringa, Kenneth Komba kuhakikisha anaandaa
mabonanza ya michezo mengi ili kuweza kupata wanamichezo mahiri watakaouletea Mkoa
sifa kubwa zaidi.
Akielezea
mafanikio ya timu hiyo Kaimu Mwenyekiti mstaafu wa Klabu SHIMIWI RAS Iringa,
Gillian Bukori amesema kuwa timu hiyo iliondoka Mkoani hapa tarehe 20/09/2012
baada ya kuagwa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa na kuitaka timu hiyo irudi na
kikombe cha ushindi.
Bukori amesema
kuwa mafanikio hayo ni kutokana na ushiriki binafsi wa Katibu Tawala Mkoa,
Getrude Mpaka, Uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na watumishi wote. Amesema kuwa
ushindi huo umechangiwa na mshikamano, upendo na kujituma kwa mtu mmoja mmoja
ndani ya timu.
Amesema
matarajio ya timu hiyo ni mwakani kuibuka na ushindi wa kwanza na kuutaka
uongozi ulioingia madarakani awamu hii kuendeleza upendo na mshikamano ili
kuleta mafanikio makubwa zaidi katika Mkoa.
Akitoa neno la
shukrani, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa,
Wamoja Ayubu amesema kuwa Mkoa utaendelea kuomba wigo kuongezwa katika bajeti
ili kuiwezesha timu ya Mkoa kushiriki kikamilifu katika michezo hiyo. Amesema Mkoa
utakuwa bega kwa bega na timu hiyo ili iendelee kufanya vizuri katika
mashindano hayo.
Akiongelea
mazoezi, Ayubu amesema kuwa mazoezi ni jambo la muhimu sana si kwa mwanamichezo
tu, bali kwa kila mtumishi na wakati wote ni muafaka kwa kufanya mazoezi si
mpaka wakati wa michezo pekee.
Wamoja ambaye
pia ni mchezi mahiri wa mchezo wa pete amesema kuwa ili timu hiyo iendelee kuwa
juu suala la kujituma ni la muhimu sana.
Timu ya kuvuta
kamba wanawake ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa iliibuka mshindi wa pili
katika mashindano hayo kitaifa yaliyofanyika Morogoro ikiwa ni hatua nzuri
zaidi ikilinganishwa na mwaka uliotangulia ilipoibuka mshindi wa nne.
Kaimu Mwenyekiti mstaafu wa Klabu ya Shimiwi Ras
Iringa Gillian Bukori akimkabidhi cheti cha ushiriki wa Mkoa mgeni rasmi Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa Gertrude Mpaka.
=30=
No comments:
Post a Comment