Tuesday, November 6, 2012

RS IRINGA WASHAURIWA KUJIANDAA KABLA YA KUSTAAFU



Watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wameshauriwa kujiandaa mapema kabla ya kipindi cha kustaafu kufika ili kuondokana na msongo wa mawazo baada ya kustaafu.

Rai hiyo imetolewa na Afisa Elimu mstaafu Mkoa wa Iringa, Salum Maduhu wakati katika salamu zake za kuwaaga watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika tafrija fupi ya kuwaaga watumishi waliostaafu na kuhamia katika vituo vipya vya kazi iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Mgeni rasmi Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka akikabidhi zawadi kwa Salum Maduhu

Maduhu amesema “ndugu zangu watumishi lazima mjiandae mapema msisubiri ubaki mwaka mmoja wa kabla ya kustaafu ndiyo uanze kujiandaa anzeni mapema”. Amesema kuwa Serikali ni nzuri sana na pia inazotaratibu nzuri kwa watumishi wake wanaostaafu kwa kuwaandalia mafao yao baada ya muda wa utumishi wa Umma. Amesema pamoja na jambo hilo jema bado suala la kujiandaa kustaafu linabaki kwa mtumishi mwenyewe.

Wakati huohuo suala la watumishi kuongea elimu limefafanuliwa vizuri na aliyekuwa Msaidizi wa Mtendaji Mkuu, Onoria Ambrose. Amesema “wafanyakazi msome, pale wafanyakazi mnaposoma hasa wale wa kada za chini kipato kinaongezeka na pindi unapostaafu mafao nayo yanaongezeka”. Aidha, amewataka wafanyakazi kujiunga na kikundi cha kusaidiana na kukuza uchumi cha MSHIKAMANO kwa ajili ya kusaidiana.

Katika taarifa fupi ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi. Gertrude Mpaka amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa tafrija fupi ya kuwaaga watumishi waliostaafu katika utumishi wa Umma katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwaaga watumishi waliohama na kuhamia vituo vingine vya kazi.

Kwa upande wa watumishi wastaafu, Mpaka amesema “ndugu wastaafu tumefanya kazi pamoja kwa muda mrefu sana, kwa upendo na ushirikiano mkubwa na kwa kufuata taratibu na kanuni zilizopo na weledi katika Utumishi wa Umma. Ushirikiano wenu ulisaidia Mkoa wetu kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Kwa msingi huo natumia fursa hii kuwashukuru kwa yale yote mazuri na utumishi uliotukuka mliyoyafanya katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kipindi chote tukiwa pamoja”.

Amesema “Sote tunatambua kwamba ninyi mlikuwa kiungo muhimu katika kufanikisha shughuli zote za Mkoa huu. Japo kuwa mmekwisha  kustaafu katika Utumishi wa Umma, bado ninyi ni nguzo muhimu sana katika mafanikio ya Mkoa wetu, tunaomba daima tuendelee kuwatumia katika ushauri na tunaamini kuwa ninyi ni hazina kubwa katika utendaji kazi kwa kuwa bado mnao uzoefu mkubwa ambao unahitajika katika kuendeleza Mkoa wetu wa Iringa” amesisitiza Mpaka.

Akiongelea watumishi waliohama, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amewakumbusha kipindi kilichopita cha utendaji kazi, na kusema “wote mtakumbuka kuwa katika kipindi chote mkiwa Watumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, tulifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kwa lengo la kuupa mafanikio Mkoa wetu. Mtakumbuka pia kuwa kuna kipindi tulifanya kazi katika mazingira magumu yote ikiwa ni kuhakikisha shughuli za Serikali zinaendelea na kufanikiwa”. Ametoa wito kwa wafanyakazi hao kuwa nidhamu na uadilifu walivyokuwa navyo katika Mkoa wa Iringa wakaviendeleze huko walipohamia na kuwa mfano wa kuigwa kwa watumishi wengine.

Watumishi waliostaafu ni;
1.
Bibi. Zahara Kimela      
Msaidizi Mtendaji Mkuu
2.
Bw. Esau Sigalla
Mchumi Mkuu
3.
Bw. Agapiti Msimbe
Mpima Ardhi Mkuu
4.
Bw. Stanley Munisi
Afisa Wanyamapori Mkuu I
5.
Bw. Robert Kinyunyu
Mlinzi Mkuu
6.
Bw. Salum Maduhu
Afisa Elimu Mkuu
7.
Bw. Ephraim Mdegela
Mlinzi Mwandamizi
8.
Bw. Cletus Karigo
Daktari wa Mifugo Mkuu
9.
Bw. Vicent James
Katibu Tawala Msaidizi Miundo mbinu
10.
Bibi. Onoria Ambrose
Msaidizi wa Mtendaji Mkuu

Watumishi waliohama ni;
1.
Bw. Barnabas Ndunguru
DAP, Wizara ya Habari, Vijana,     Utamaduni na Michezo.

2.
Bw. Leornad Msigwa
Afisa Elimu Sekondari,
DED – Iringa
3.
Dkt. Ezekiel Mpuya
Mganga Mkuu wa Mkoa,
RAS Dodoma
4.
Bibi.  Grace Manga
Mhasibu Daraja la II
RAS Morogoro



No comments:

Post a Comment