Wednesday, August 22, 2012

...AMIA HUKU DIGITALI



Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa elimu kwa umma ni nyenzo muhimu sana katika kuwaandaa wananchi kuhama kutoka katika mfumo wa utangazaji wa analojia na kuingia katika mfumo wa digitali.

Ameyasema hayo katika mkutano wa viongozi wa mkoa wa Iringa kuhusiana na mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka analojia kwenda digitali uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu Huria, tawi la Iringa.

 Mkuu wa Mkoa wa Iringa akisoma hotuba yake

Picha ya Pamoja ya washiriki wa Warsha hiyo

Amesema katika kufanikisha jitihada hizo, “umeonekana umuhimu wa kuelimisha umma kwa kushirikisha wizara, idara za Serikali pamoja na wananchi wote ili kuweza kufanikisha mabadiliko haya kwa ufanisi bila kuathiri upatikanaji wa huduma za utangazaji nchini”. Ameishauri kamati maalumu ya kitaifa inayofanya kazi ya kuwaelimisha wananchi nchini juu ya mabadiliko ya teknolojia ya utangazaji kuhakikisha wananchi wengi wanapata elimu hiyo ili kuwaandaa na mabadiliko hayo. Amesema maana ya mabadiliko ya teknolojia, matarajio ya baada ya mabadiliko na wajibu wa mwananchi katika kufanikisha mabadiliko hayo ni mambo ya muhimu kutiliwa mkazo katika utoaji wa elimu kwa wananchi.

Akiongelea Sensa ya Watu na Makazi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ametoa wito kwa washiriki hao kuuelimisha umma juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi. Amesema “natoa wito kwenu washiriki wa mkutano huu hasa waandishi wa habari kutumia nafasi hii kuhimiza jambo hili na kutumia muda wenu na vyombo vyenu kuwaelimisha wananchi ili waweze kushiriki katika zoezi hili na kulifanya liwe la manufaa na kuleta tija katika Mkoa wetu wa Iringa na Taifa kwa ujumla” alisisitiza Dkt Christine.
=30=

No comments:

Post a Comment