Friday, March 16, 2012

MAAFISA KILIMO WATAKIWA KUFANYA MABADILIKO

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika amewataka maafisa kilimo na wadau wa sekta hiyo kufanya mabadiliko makubwa katika kukuza sekta hiyo ili iwe ya kisasa na kuifanya iwanufaishe wananchi wengi zaidi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Prof. Jumanne Maghembe, wakati akifungua mkutano wa maafisa kilimo wa Tanzania bara, uliofanyika katika hoteli ya royal village, katika Manispaa ya Dodoma.

Prof. Maghembe amesema kuwa asilimia 77.5 ya wananchi wanaokadiriwa kufika mil. 40 wanategemea sekta ya kilimo katika kuendeleza maisha yao na kati yao asilimia 22.5 ndiyo wanaofanya kazi katika sekta hiyo.

Amesema pamoja na ukubwa wa asilimia ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo  bado kilimo kinachangia asilimia 34 tu ya fedha za kigeni nchini. Katika mchango wa kilimo katika pato la taifa, kinachangia asilimia 24 pekee. Amesema “bado kazi inatakiwa kufanywa na sisi tuliomo humu ndani, tumeandaliwa vizuri kitaaluma ili tuweze kutekeleza hili, kushindwa tunaliangusha taifa”.    

Prof. Maghembe amesema kuwa kilimo nchini kinakua kwa asilimia 4.2 tofauti na lengo la kitaifa la kilimo kukua kwa angalau asilimia 6 kwa mwaka.

Pamoja na kuhimiza kilimo cha umwagiliaji, Waziri wa kilimo, Chakula na Ushirika amesema “suala si kuongeza maeneo ya kulima, bali ni kuongeza uzalishaji katika maeneo tunayolima”.

Akiongelea vikwazo vinavyoikabili sekta ya kilimo, amesema kuwa masoko yasiyo ya uhakika dunia na kuwataka wadau hao kujipanga katika kukuza kilimo ili kiweze kuzinufaisha nchi zenye upungufu wa chakula na kuzifanya zisifikirie kununua chakula sehemu nyingine zaidi ya Tanzania.

Akichangia katika mkutano huo huku akisikilizwa kwa umakini mkubwa na mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa nchi haiwezi kuwa na mafanikio katika sekta ya kilimo bila kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Amesema ni vema juhudi zikawekwa katika kufufua kilimo cha umwagiliani pamoja na kuimarisha skimu za umwagiliaji ili kilimo kiweze kushamiri.

Akichangia katika upatikanaji wa soko, Dk. Ishengoma amesema kuwa soko ni changamoto kuwa kwa kufanikisha shughuli za kilimo. Amesema ukitangaza uhakika wa soko la mazao mapema wakulima watalima kwa nguvu kwa sababu watakuwa na uhakika na soko. Akitolea mfano katika mkoa wake wa Iringa, amesema kuwa mkoa huo umehimiza kilimo cha zao la mtama kwa wingi ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa chakula, muitikio umekuwa mzuri baada ya kuwa na uhakika wa soko.

Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni upungufu wa fedha za ufuatiliaji, hatua inayowakwamisha wataalamu wa kilimo katika kutekeleza majukumu yao katika sekta ya kilimo.
=30=

No comments:

Post a Comment