Friday, March 16, 2012

TANZANIA YABORESHA HUDUMA ZA MAJI

Na.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ukiwemo mpango wa kuboresha usimamizi na rasilimali za maji na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji safi, usafi wa mazingira na maji kwa ajili ya umwagiliaji.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji kitaifa mkoani Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, aliyemuwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika amesema kuwa “Serikali kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini -MKUKUTA, na mabadiliko mbalimbali ya kisera na kimfumo, imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikiwemo mpango wa kuboresha usimamizi na rasilimali za maji, kuboresha upatikanaji wa huduma za majisafi, usafi wa mazingira na maji kwa ajili ya umwagiliaji”.

Amesema kuwa kwa sasa Serikaili inatekeleza mpango wa pamoja wa matumizi ya rasilimali za maji kupitia ofisi zote tisa za mabonde nchini. Amesema pindi mpango huo utakapokamilika utaainisha njia za matumizi bora ya rasilimali maji.

Amesema “katika kuhakikisha rasilimali ya maji inatumika kwa manufaa ya taifa na usalama wa chakula nchini unakuwepo, ninawaomba viongozi wenzangu, vyombo vinavyosimamia rasilimali maji kama vile Mamlaka za Maji, Ofisi za Maji za Mabonde, Vyombo vya Watumiaji Maji na wananchi kwa ujumla kujiandaa kuzikabili changamoto na vihatarishi nilivyotaja”.

Ameitaka jamii kushirikiana katika kuhifadhi, kutunza na kuendeleza mfumo mzima wa maji kuanzia kwenye vyanzo, uzalishaji na ugawaji kwa kuzingatia ongezeko la matumizi ya maji.

Mkoa wa Iringa ni mwenyeji wa maadhimisho ya 24 ya wiki ya maji kitaifa yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo ‘maji kwa usalama wa chakula’, shughuli mbalimbali za sekta ya maji pamoja na maonesho zitafanyika katika uwanja wa Samora na maeneo mengine.
=30=

No comments:

Post a Comment