Saturday, February 28, 2015

DC MBONI AAPISHWA RASMI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa IRINGA
Ushirikishaji wananchi na makundi mengine katika jamii ni njia rahisi ya kuleta tija katika utekelezaji wa Ilani ya CCM na miradi ya maendeleo mkoani Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza muda mfupi baada ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa. 
Mhe. Mboni Mhita (kulia) walio kaa na Mhe. Amina Masenza (kushoto). Waliosimama ni Maafisa waandamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa
 Masenza amesema kuwa katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 na miradi yote ya maendeleo katika Wilaya na Mkoa dhana ya ushirikishaji wananchi na wadau wengine ni muhimu sana katika kuleta tija ya kazi. Amesema wananchi na makundi mengine yanaposhirikishwa uelewa wa pamoja unakuwepo na kufanya utekelezaji wake kuwa ni jukumu la jamii nzima. Amesema kuwa mara nyingi mtafaruku na wananchi unatokea pale ambapo ushirikishwaji unakuwa mdogo au hakuna kabisa.
Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya kusoma kwa umakini nakala ya wajibu wa Mkuu wa Wilaya na kuuelewa kwa sababu ndiyo muongozo katika utendaji kazi wa Mkuu wa Wilaya. Amesema kuwa hakuna jambo lisilowezekana na kumtaka kutumia vizuri vyombo vya usalama na wataalamu waliopo katika Wilaya ya Mufindi. Aidha, amemtaka kufanya kazi bega kwa bega na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi ili kazi yake iwe nyepesi. Amesema kuwa Kamati hiyo inawajibu wa kumshauri na kumsaidia katika kutekeleza majukumu katika Wilaya ya Mufindi.
 Mkuu wa Mkoa amesema kuwa wananchi wote wanamatumaini na Wakuu wa Wilaya katika kutatua matatizo yao. “Wewe ni lulu, wananchi wote wataangaika sehemu zote watakazokwenda lakini wakifika kwako watasema hapa tumefika na hapa ndiyo mwisho. Unamwambia mwananchi nenda mahakamani hataki, nenda polisi hataki nenda kwa Mkurugenzi hataki anajua wewe ndiye utaweza kumsimamia na wewe peke yako ndiye unaweza.” Alisisitiza Masenza.
Amesema kuwa wananchi wengi wanamatumaini sana na Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa sababu wanamajibu ya papo kwa papo kwa matatizo ya wananchi kwa vile vyombo walivyonavyo vinawafanya kuwa na majibu.
Akitoa shukrani zake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mboni Mhita amemshukuru Mhe. Rais kwa imani aliyonayo kwake na kumteua katika nafasi hiyo. Aidha, ameomba ushirikiano na ushauri kadri inavyowezekana ili kazi yake iwe rahisi. Amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kumpatia nasaha na vitendea kazi. “Mbali na vitabu ambavyo umenipa vya Ilani pamoja na Katiba, maneno yako yamekuwa na uzito sana naomba nikuahidi kwamba nitayazingatia na pindi nitakapoona kwamba nimekwama au nahitaji ushauri basi sitasita kuja kwako kuomba ushauri.” Alisisitiza Mboni.
Tukio hilo la kuapishwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi limeshuhudiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, familia ya Mboni, watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Mufindi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.
=30=

No comments:

Post a Comment