Wednesday, January 17, 2018

IRINGA NA MPANGO WA KUBORESHA UTALII



Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa

Mkoa wa Iringa umeandaa mpango wa kuboresha maonesho ya utalii karibu kusini ili kuweza kuwavutia watalii wengi kutembelea vivutio vya utalii na kufurahia mandhari iliyopo katika vivutio hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi waliotembelea Mkoa wa Iringa kwa ziara ya mafunzo.
 
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Iringa na timu kutoka chuo cha Taifa cha Ulinzi
Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa ni kitovu cha utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. Maonesho ya utalii karibu kusini yanatumika kukuza sekta ya utalii kwa mikoa ya nyanda za juu kusini. “Maonesho ya utalii karibu Kusini yanatumika kama mkakati maalum wa kufungua sekta ya utalii kwa ukanda wa Kusini ambao umejaa fursa na vivutio vya kipee katika utalii.

Alitolea mfano maporomoko ya maji ya Kihansi ambapo wanapatikana vyura wa kipekee wanaozaa tofauti na vyura wengine wanaotaga mayai.

Mkoa wa Iringa ukiwa mratibu umeandaa mipango ya kuboresha maonesho haya kwa kutenga eneo la Kihesa Kilolo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya utalii karibu kusini. Eneo hili litatumiwa na wadau wa utalii na wadau wa maendeleo kujenga miundombinu kwa ajili ya kuonesha huduma na bidhaa za sekta ya utalii” alisema Masenza.

Akitoa neno la shukrani, kiongozi wa wajumbe kutoka chuo cha Taifa cha ulinzi Capt. Msafiri Hamisi alipongeza kwa mapokezi ya Mkoa na kazi zinazofanywa na Mkoa za kuwahudumia wananchi na kuwaletea maendeleo. Aidha, aliahidi wanafunzi wa chuo cha Taifa cha ulinzi kuwa balozi wazuri kwa mkoa wa Iringa.

Mkoa wa Iringa ulifanya maonesho ya kuendeleza utalii ya karibu Kusini kwa miaka miwili mfululizo (mwaka 2016 na 2017) kwa kushirikisha mikoa ya nyanda za juu kusini ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Katavi.
=30=

No comments:

Post a Comment