Thursday, December 21, 2017

UBIA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI WAONGEZA UFANISI SAGCOT


Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mafanikio ya ubia baina ya sekta ya umma na sekta binafsi yamebadilisha fikra na kuongeza ufanisi kwa watendaji wa sekta ya umma katika mikoa ya Iringa na Njombe katika utekelezaji masuala ya ubia.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya mafanikio ya SAGCOT kwa Mkoa wa Iringa wakati wa ziara ya Katibu mkuu Ofisi ya waziri mkuu anayehusika na sera na mipango mkoani Iringa jana.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu akisoma taarifa ya Mafanikio ya SAGCOT kwa Mkoa wa Iringa

Ayubu alisema “moja ya mafanikio ya ubia uliyopo ni kubadilika kwa fikra na kuongezeka kwa ufanisi kwa watendaji wa sekta ya umma katika utekelezaji wa masuala yanayohusu ubia na sekta binafsi”. 

Alisema kuwa Mkoa uliweza kufuatilia changamoto mbalimbali na kufanikisha upatikanaji wa umeme kwenye kiwanda cha kusindika nyanya kiitwacho Darch Industries Ltd. Aliongeza kuwa upatikanaji wa barabara kutoka kiwanda hicho cha kusindika nyanya hadi barabara kuu ya Iringa-Mbeya uliwezeshwa. “Upatikanaji wa maeneo kwenye vijiji vinavyozalisha zao la nyanya kwa ajili ya kujenga vituo vya kukusanyia nyanya. Vituo vinane vimejengwa na wabia wa kiwanada cha kusindika nyanya” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa alizitaja juhudi zilizofanywa na Mkoa kuwa ni pamoja na kutatua mgogoro wa matumzi ya maji kati ya muwekezaji (Silverlands) na wananchi ambapo hati ya makubaliano ya matumizi ya maji ilisainiwa na pande zote mbili. Pia, Mkoa umefanikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika kiwanda cha kusindika chai cha Unilever.

Kongani ya Ihemi (Iringa na Njombe) inajumuisha wilaya za Iringa, Kilolo, Mufindi, Njombe na Wanging’ombe ilianza utekelezaji chini ya mpango wa SAGCOT mwaka 2015 ikiwa ya kwanza kati ya kongani sita za SAGCOT.

=30=

No comments:

Post a Comment