Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Halmashauri
ya Manispaa ya Iringa imekalimisha ujenzi wa barabara ya St. Dominic kwa
kiwango cha lami kwa zaidi ya shilingi 290,000,000.
Kauli
hiyo ilitolewa na Kaimu Mhandisi wa Manispaa ya Iringa, Mhandisi Richard Moshi
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kazi za matengenezo ya barabara kwa mwaka
wa fedha 2015/2016 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa
kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa mjini Iringa.
Mhandisi
Moshi alisema kuwa katika mpango wa mwaka, upatikanaji wa huduma za miundombinu
na mawasiliano kuboreshwa, ilipangwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami
barabara ya St. Dominic na kipande cha Ilala km 0.76 kwa kiwango cha lami.
Alisema kuwa katika utekelezaji wa ujenzi huo, fedha iliyotengwa ni shilingi
348,614,279.40 wakati fedha iliyotumika ni shilingi 290,521,317.91 na mradi
umekamilika na upo katika muda wa matazamio.
Mhandisi
Moshi alieleza ujenzi wa mifereji eneo la Mawelewele kata ya Mwangata km 2.3 na
kuweka changarawe km 1.0 mtaa wa Kibarabara. “Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 85 kwa gharama ya shilingi
290,694,241” alisema Mhandisi Moshi.
Akiongelea
matengenezo ya muda maalum ya barabara ya Makanyagio 1.5 km, shughuli
iliyofanyika ni kuchimba mtaro na matengenezo hayo yamefikia asilimia 15.
Aidha, fedha, zilizotengwa kwa matengenezo hayo ni shilingi 84,700,518.
Halmashauri
ya Manispaa ya Iringa ina mtandao wa barabara zenye urefu wa km 525.969, kati
ya barabara hizo, km 50.165 ni barabara kuu na barabara za Mkoa ambazo
zinahudumiwa na Wakala wa barabara nchini (TANROADS) kwa matengenezo. Km
475.804 ni barabara zilizo chini ya mamlaka ya Manispaa na matengenezo yake
hufanywa na Halmashauri ya Manispaa. Kati ya km 19.483 ni za lami, km 125.439
ni za changarawe na km 341.057 ni za udongo.
=30=
No comments:
Post a Comment