Wednesday, September 13, 2017

KARIBU KUSINI NA SIDO KULETA WANYAMAPORI HAI MAONESHO YA IRINGA



Na Mwandishi Maalum, IRINGA
Kamati ya maandalizi ya maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini imetakiwa kuhakikisha wanyamapori hai wanakuwepo katika maonesho hayo.

Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha pamoja cha viongozi wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini cha maandalizi ya maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kanda ya nyanda z juu kusini kilichofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha nje kidogo ya mji wa Iringa.
Picha ya pamoja na wakuu wa Mikoa na watalaam katika Hifadhi ya taifa ya Ruaha

Mheshimiwa Masenza alisema kuwa wanyamapori hai ni muhimu katika maonesho hayo kwa sababu wananchi wengi wanapenda kuwaona wanyamapori hai moja kwa moja. Aidha, alishauri kasi ya kufuatilia wanyamapori hao inayofanywa baina ya kamati ya maandalizi na wizara ya Maliasili na Utalii iongezwe.

Katika taarifa ya kamati ya maandalizi iliyowasilishwa na Fikira Kisimba alisema kuwa ufuatiliaji unaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kupata wanyama hao. “Wizara imetoa bajeti elekezi ambapo mikoa inawajibika kuchangia jumla ya shilingi 4,000,000 kukodi mabanda yote manne ya wanyama” alisema Kisimba. 

Akiongelea wadau waliothibitisha kushiriki katika maonesho hayo, alisema kuwa wadau 312 wamethibitisha kushiriki. Aliwataja baadhi ya wadau hao kuwa ni wizara ya Maliasili na Utalii; wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezeji; wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; na TATO. Wengine ni KILI FAIR; Wakala wa Misitu Tanzania; Ngonga beach; UPL Link Mbeya; Uyole cultural Enterprises; Baraza la Biashara la Taifa; Heifer International; Care International na Wajasiliamali 300.

Wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini walioshiri ziara hiyo ni Amina Masenza mkuu wa Mkoa wa Iringa, Luteni (Mst) Chiku Galawa Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Christopher Ole Sendeka mkuu wa mkoa wa Njombe.

Maonesho ya Utalii yatafanyika pamoja na Maonesho shughuli za Viwanda Vidogo (SIDO) kanda ya nyanda za juu kusini kwa Mwaka 2017.  Maonesho haya yamepangwa kufanyika kuanzia tarehe 29/09/2017 hadi tarehe 02/10/2017.
=30=

No comments:

Post a Comment