Kampuni za mbolea
zaidi ya 10 zimejitokeza kuhudumia wakulima katika Wilaya ya Iringa kwa ajili
ya kusambaza vocha za pembejeo za kilimo kwa mwaka 2012/2013 na 2013/2014.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa utoaji wa pembejeo zenye ruzuku kwa msimu wa kilimo
wa mwaka 2011/2012 na maandalizi ya kilimo msimu wa mwaka 2012/2013 katika
kikao cha kamati ya pembejeo cha mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo, Mifugo na
Ushirika wa Wilaya ya Iringa, Lucy Nyalu amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa imepokea utaratibu mpya kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wa
usambazaji wa pembejeo zenye ruzuku ya Serikali kwa wakulima wa mahindi na
mpunga kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2012/2013.
Amesema kuwa
utaratibu wa kutumia vocha utaendelea ila mawakala watakaosambaza pembejeo hizo
kwa wakulima wanufaika na kampuni ya pembejeo ndiyo itasambaza pembejeo hizo
badala ya kamati ya pembejeo ya wilaya kama
ilivyokuwa awali.
Amesema lengo la
kampuni za pembejeo kupewa jukumu la kuteua mawakala ni kuhakikisha pembejeo
zenye ubora zinawafikia wakulima kwa wakati muafaka. Amesema kuwa kazi ya
kamati ya pembejeo ya wilaya itakuwa ni kusimamia na kufuatilia utaratibu mzima
wa pembejeo katika mchakato wote.
Lucy amesema
jumla ya kampuni 13 za mbolea na mbegu zimejitokeza kuhudumia wakulima wa
Wilaya ya Iringa. Amesema makampuni hayo yameteua mawakala wawakilishi saba na
mawakala wasaidizi 46. Akiongelea uhamasishaji wa matumizi ya mbolea ya
minjingu mazao pamoja na utaratibu wa usambazaji wa vocha za pembejeo za kilimo
kwa wakulima kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na 2013/2014 umefanyika katika
vijiji vya Nyabula, Lupembelwasenga, Usengelindeti, Makombe, Kihanga, Ng’enza,
Magulilwa na Tagamenda. Uhamasishaji huo
unaendelea sambamba na usambazaji wa vocha za pembejeo.
Wakati huohuo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa
imepokea mgao wa pembejeo zenye ruzuku kwa mwaka 2012/2013 zenye thamani ya
shilingi 1,828,654,000. Akielezea aina ya pembejeo hizo, Afisa Kilimo, mifugo
na ushirika amesema kuwa mbolea ya kupandia vocha (22,000), mbolea ya kukuzia
(22,000), mbegu ya mahindi (chotara) (5,409),mbegu ya mahindi mchanganyiko
(9,309), mbegu ya mpunga (7,282).
Lucy ameyataja mafanikio yaliyotokana na mfumo wa
vocha kuwa ni upatikanaji wa pembejeo katika ngazi ya kijiji umefikiwa ambapo
wakulima wanaweza kununua pembejeo katika maeneo ya vijiji vyao. Mafanikio
mengine ameyataja kuwa ni ongezeko la uzalishaji kutoka gumia 3-5 za mahindi
hadi kufikia wastani wa gunia 12-22 kwa ekari, kwa zao la mpunga ongezeko
kutoka gunia 8-10 hadi kufikia wastani wa gunia 16-25. Aidha, idadi ya wakulima wanaolima kitaalamu
imeongezeka na matumizi ya pembejeo kwa wakulima yameongezeka.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt.
Christine Ishengoma amekiaarifu kikao hicho kuwa msimu wa kilimo umefika na
kuwa mvua zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi na
wakulima wameanza kupanda. Aidha, aliwataka wataalamu wa kilimo kuwa karibu na
wakulima katika kuwafundisha na kuwaelekeza mbinu bora za kilimo.
=30=
No comments:
Post a Comment