Serikali ya Japan
imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika sekta mbalimbali hasa sekta ya afya na kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa,
Dkt. Christine Ishengoma akimkabidhi kitabu cha profile ya Mkoa wa Iringa
Balozi wa Japan nchini Tanzania
Ahadi hiyo
imetolewa na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaki Okada alipotembelea ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika ziara iliyolenga kusaini mkataba wa ukarabati
wa hospitali ya Tosamaganga iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Balozi Okada
amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuhakikisha uchumi
unakuwa kwa kasi zaidi kwa kukuza biashara baina ya nchi mbili hizo. Amesema
kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania wanategemea kilimo, ni lazima
kipato chao kiongezeke ili waweze kunufaika na kilimo hicho kama shughuli yao kuu ya kiuchumi.
Amesema kuwa Serikali yake inao mpango wa kuisaidia sekta ya kilimo nchili ili
kuhakikisha kilimo cha mpunga kinaongezeka mara dufu kwa kuwa nchi ya Japan
inasifika kwa uzalishaji wa mpunga duniani.
Aidha,
amezipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo
wananchi wake na kuahidi kuziunga mkono juhudi hizo kwa karibu.
Awali katika
salamu za Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amesifu juhudi za
Serikali ya Japan katika kusaidia maendeleo kwa mkoa wa Iringa na kusema ni
juhudi za kupongezwa sana .
Amesema kupitia misaada ya Japan, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imeweza
kupata ufadhili katika utekelezaji wa miradi ya afya, elimu, kilimo, maji na
umwagiliaji.
Akiongelea
maambukizi ya virusi vya ukimwi na ukimwi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa
kwa kujibu wa utafiti wa mwaka 2008, mkoa wa Iringa ulikuwa na takribani
asilimia 16 ya maambukizi, kiwango ambacho ni karibu mara tatu ya kiwango cha
maambukizi kitaifa. Amesema kuwa hali hiyo haikubaliki na zinaihitajika juhudi
za pamoja kati ya Tanzania
na Japan katika kuendeleza mapambano hayo. Aidha, amezipongeza juhudi za
Serikali ya Japan za kuisaidia Tanzania
katika sekta ya afya na ustawi wa jamii kupitia miradi mbalimbali kwa lengo la
kuboresha afya ya mama na familia katika
mkoa wa Iringa.
Balozi wa Japan
nchini Tanzania
yupo mkoani Iringa kwa ajili ya utiaji saini mkataba wa ukarabati wa hospitali
ya Tosamaganga unaogharimu dola za kimarekani 123,339 kwa lengo la kuongeza
ubora wa huduma za afya na kupunguza vifo vya wanawake na watoto mkoani Iringa.
=30=
No comments:
Post a Comment