Monday, September 3, 2012

RCC SIMAMIENI MIRADI YA MAENDELEO



Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa wametakiwa kusimamia vizuri miradi na fedha za Serikali ili kudhibiti matumizi mabaya na hoja zinazoweza kujitokeza kutokana na kutokusimamia vizuri fedha na miradi hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, wakati akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Siasa ni Kilimo katika Wilaya ya Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma (katikati) akiendesha kikao cha RCC


Dkt. Christine amesema kuwa katika agenda zitakazojadiliwa ni utekelezaji wa Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. “Ninalowasihi ndugu wajumbe, kwa mwaka huu, kuanzia sasa ni kusimamia miradi na fedha ambazo Halmashauri hupewa na Serikali, ili kudhibiti ubadhilifu wa fedha na hoja zinazoweza kujitokeza” asilisitiza Dkt. Christine. Aidha, aliwashauri kutokuanzisha miradi mipya wakati miradi ya zamani haijakamilika na kuwataka kumaliza miradi viporo kwanza ndipo waanzishe miradi mipya.

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, aliwashauri wajumbe wa kikao hicho kuwashauri wakulima wanaoishi katika maeneo yenye upungufu wa mvua, kulima mazao yanayovumilia ukame. Amesema “nichukue fursa hii kuwaomba kufikisha ujumbe kwa wakulima wanaoishi maeneo yenye upungufu wa mvua, kuwa ni vizuri wakulima walime mazao ya mtama na alizeti ambayo yanavumilia ukame”.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa alitumia kikao hicho kuwataka wajumbe kusimamia suala la utunzaji wa mazingira ambayo kwa sasa yanaharibiwa kwa kasi kubwa na shughuli za binadamu.   
Wakati huo huo, Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi 950,000,000 kwa mwaka wa fedha 2011/ 2012.

Akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na bajeti kwa kipindi cha Julai-Juni, 2011/ 2012, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Nuhu Mwasumilwe amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012, Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi 903,000. Amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2012 jumla ya shilingi 950,895,762 zimekusanywa kwa mchanganuo ufuatao, marejesho ya mishahara ni shilingi 949,591,700, kodi ya pango la nyumba ni shilingi 636,238 na ada ya ufuatiliaji shilingi 19,000.

Mwasumilwe amesema kwa upande wa Serikali za Mitaa, katika kipindi cha mwaka 2011/ 2012, Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa zilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 8,342,138,599 kutoka katika vyanzo vyake vya mapato vya ndani. Amesema hadi kufikia mwezi Juni, 2012 jumla ya shilingi 7,358,634,981 zimekusanywa ambazo ni sawa na asilimia 88.2 ya lengo.

No comments:

Post a Comment