Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amezindua kamati ya kuendeleza Utalii
na Mazingira mkoani Iringa na kuitaka ijiwekee malengo mahususi ya kuendeleza utalii katika
mkoa huo na ukanda wa kusini kwa ujumla wake.
Dkt.
Christine amesema kuwa lengo la kuunda kamati hiyo ni kuufanya utalii uweze
kushamiri katika ukanda huo kama ulivyoshamiri katika ukanda wa kaskazini na
kusisitiza kuwa mkoa wa Iringa uliteuliwa kuwa kitovu cha utalii kwa ukanda wa
nyanda za juu kusini.
Ameitaka
kamati hiyo iliyosheheni wataalamu mbalimbali kutoka katika sekta ya utalii,
mazingira, habari na sekta mtambuka kufanya kazi kwa kujituma na kujitoa ili
kufanikisha malengo ya kamati hiyo.
Mkuu wa Mkoa
ameyataja majukumu ya Kamati hiyo kuwa ni pamoja na kujadili mawazo, maoni na
mbinumbalimbali za kuhamasisha na kuendeleza utalii mkoani Iringa. Kuratibu
maonesho, matukio na vikao vya wadau wa utalii mkoani Iringa. Majukumu mengine
ameyataja kuwa kuandaa mipango mikakati na shughuli za kuhamasisha na kuendeleza
utalii mkoani Iringa pamoja na kufuatilia upatikanaji wa eneo la maonesho ya
utalii. Mengine ni kufanya jitihada za kutambua vivutio vya utalii vilivyopo
mkoani Iringa na kuvitangaza ndani na nje ya nchi na kusaidiana na vyombo vya
usalama na usafiri kuhakikisha kuwepo kwa usalama na usafiri wa watalii wa
ndani na nje ya nchi.
Katibu wa
Kamati hiyo, Risala Kabongo alishauri kuwa dhana ya utalii ni vema ikajikita
katika kuhusisha kilimo, maji na usalama. Amesema utalii ni sekta mtambuka
hivyo unahusisha mambo sekta mbalimbali za kimaendeleo.
Wakati
huohuo, Afisa Utalii Manispaa ya Iringa, Fidelis Mrute alihusisha nafasi ya
idara ya uhamiaji katika kuimarisha usalama katika sekta ya utalii. Amesema
idara hiyo ni muhimu katika kubaini kati ya mtalii halisi hasa wa nje ili
kutofautisha na watu wasiokuwa na nia njema na sekta ya utalii.
Mkuu wa Mkoa
wa Iringa ameteua kamati ya kuendeleza utalii na Mazingira kwa mkoa wa Iringa
na kamati hiyo itahudumu kwa muda wa miaka mitatu.
=30=
No comments:
Post a Comment