Wananchi Mkoani Iringa wametakiwa
kuhakikisha kuwa wanahesabiwa ndani ya siku saba za zoezi la kuhesabu watu ili
kuiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na kupanga mipango shirikishi ya
maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Dkt. Christine Ishengoma, katika mahijiano ya moja kwa moja na Redio
Furaha ya mjini Iringa kupitia kipindi maarufu cha Nyota ya Asubuhi.
Dkt. Christine amesema “msisubiri
mpaka siku saba zifike, ukiona imefika siku ya tano yaani tarehe 30.08.2012
hujahesabiwa toa taarifa kwa kiongozi wa Serikali katika eneo lako”. Amesema
kuwa wale wanaokaa mijini watoe taarifa zao kwa wenyeviti wao wa mitaa na wale
wanaokaa vijijini wahakikishe wanatoa taarifa zao kwa wenyeviti wa vijiji.
Akifafanua kuhusu changamoto ya
lugha katika kufanikisha zoezi hilo, Mkuu wa Mkoa amezishukuru juhudi ya hayati
baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere za kuwaunganisha watanzania wote kwa lugha
ya kiswahili. Amesema kuwa kwa wale wachache itakaotokea hawafahamu lugha hiyo
ni vema wakawaandaa watu wanaowaamini na kuwa wakalimani wao ili kufanikisha
zoezi hilo.
Wakati huohuo, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, amewatoa hofu wananchi wote wanaotaka kulihusisha zoezi la Sensa ya Watu
na Makazi na dhana ya u-freemarson kuwa zoezi hili hali uhusiano wowote na
dhana hiyo na kuwataka wananchi kuwapuuza wale wote wanaotumia dhana hiyo kwa
ajili ya kutaka kukwamisha zoezi hilo.
Akijibu swali juu ya imani ya
Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anahesabiwa ndani ya kipindi cha
siku saba na upungufu wa makarani wa Sensa, Mratibu Msaidizi wa Sensa Mkoa wa
Iringa, Conrad Millinga amesema kuwa Serikali haina wasiwasi juu ya zoezi hilo
kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Amesema kuwa katika Sensa ya Majaribio
iliyofanyika tarehe 02 Oktoba, 2011, ilikamilika ndani ya siku saba na
ilifanyika katika maeneo 44 ya kuhesabu watu katika mikoa tisa, mikoa saba ya
Tanzania Bara na mikoa miwili ya Zanzibar. Amesema kuwa makarani wapo wa kutosha
na katika maeneo yaliyo na idadi kubwa ya kaya wameongezwa makarani wa ziada
ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakamilika katika muda uliopangwa na kwa
ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment