IRINGA
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika
kutoa na kuboresha huduma katika sekta ya afya nchini kwa lengo la kumuhudumia
vizuri mwananchi.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Dkt. Christine
Ishengoma katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya
Iringa, Dkt. Leticia Warioba wakati wa ufunguzi wa jengo la huduma ya upasuaji
wa macho pamoja na kituo cha huduma ya kupima na kutengeneza miwani katika hospitali
ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Dkt. Christine amesema kuwa Serikali
itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha
wananchi wanapata huduma bora za afya kwa sababu Serikali peke yake haiwezi
kutekeleza jukumu hilo.
Akiongelea ufunguzi wa jengo la huduma
ya upasuaji wa macho pamoja na kituo cha huduma ya kupima na kutengeneza miwani,
amesema kuwa shughuli hiyo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 70 zikiwa ni
ukarabati wa jengo la huduma ya upasuaji. Amesema shilingi milioni 35
zimetumika kununua vifaa tiba vilivyopo katika kituo cha kupima na kutengeneza
miwani zikiwa ni misaada kutoka mashirika ya Sightsavers na taasisi ya Brien
Holden Vision.
Amesema kuwa mashirika hayo yameonesha dhamira ya wazi ya
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza
Sera ya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuimarisha huduma
za jamii.
Aidha, amewataka watumishi wa idara ya afya hasa huduma za macho
kuhakikisha wanatumia msaada huo kwa malengo yaliyokusudiwa. Kwa wasimamizi wa huduma
za afya katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kuhakikisha vifaa vyote
vilivyotolewa na wadau vinaingizwa katika leja ya hospitali na kutunzwa kwa
kufanyiwa matengenezo na matengeneza kinga kama inavyotakiwa ili viweze kutoa
huduma kwa muda mrefu.
Katika taarifa ya huduma za mradi
jumuishi wa macho Iringa iliyowasilishwa na Daktari bingwa wa macho katika hospitali
ya rufaa ya mkoa wa Iringa, Dkt. George Kabona amesema kuwa shughuli za mradi
jumuishi wa huduma za macho mkoani Iringa ulianzishwa mwaka 1998 kwa
ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na shirika lisilo la
kiserikali la Sightsavers.
Amesema kuwa lengo kubwa la mradi
huo ni kuhakikisha watu wote wenye upofu unaozuilika wanapatiwa huduma ya
kuepukana na upofu huo na wale wenye upofu usiozuilika wanapatiwa elimu bora
hasa watoto.
Dkt. Kabona amezitaja shughuli za mradi
huo zilizogawanyika katika sekta tatu kuwa ni afya ya macho, elimu jumuishi na
utengamao.
Akiongelea mafanikio ya mradi huo, amesema kuwa sekta hiyo
imepata mafanikio makubwa na kuyataja kuwa ni pamoja na kuweza kuwaona na
kuwapatia huduma wagonjwa 76,471 katika mkoa mzima wa Iringa kati ya mwaka
2009-2011. Mafanikio mengine ni kufanyika kwa upasuaji kwa wagonjwa 6,280
katika kipindi hicho.
=30=
=30=
No comments:
Post a Comment