Thursday, January 18, 2018

WAKUU WA SHULE NA WALIMU WAKUU WATAKIWA KUTHIBITISHA KWA BARUA MICHANGO INAYOENDELEA KATIKA SHULE ZAO



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewataka wakuu wa shule za sekondari na msingi kuthibitisha kwa barua iwapo kuna michango yeyote inayoendelea katika shule zao kinyume na maelekezo ya serikali.

Agizo hilo amelitoa leo katika kikao cha dharura na wakuu wa shule na walimu wakuu kufuatia agizo la Rais w Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa jana kuhusu michango katika shule nchini.
 
Walimu waliohudhuria kikao cha dharura cha Mkuu wa Mkoa wa Iringa

Serikali imekwisha elekeza kuwa tunakwenda na elimu bila malipo. Mtu yeyote nayekwenda kinyume na hilo anakwenda kinyume na maelekezo ya serikali. Ni Rais aliyetoa amri hii yeye ndiye mwenye usemi wa mwisho katika mambo yote ya Taifa hili. Yeyote anayekiuka hili atakuwa anafanya kwa dharau” alisema Masenza.

Alisema kuwa waraka wa elimu Namba 3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimu ya msingi bila malipo ulitoa maelekezo ya utekelezaji wa jambo hilo.

Alisema kuwa alikwisha kuwa iwapo kuna hitaji lolote katika shule, libainishwe na jamii na jamii yenyewe ndiyo isimamie utekelezaji wa jambo hilo nje ya utaratibu wa mwalimu mkuu na walimu wengine.

Nimewaita hapa nijiridhishe, nitamtaka kila mwalimu mkuu wa shule ya msingi na sekondari kwa mkono wake aandike barua kwa mkuu wa Mkoa kuthibitisha kwamba ama upo mchango unaoendelea katika shule yake ama hakuna. Barua zenu zote tutazipitia moja baada ya nyingine. Baada ya hapo tutakuwa na ukaguzi na kuongea na bodi na kamati za shule ili zitumbie kama wanayo michango, michango hiyo iliidhinishwa na nani, ni kiasi gani na kwa madhumuni gani?” alihoji mkuu wa Mkoa.

Aliongeza kuwa eneo lolote litakalobainika kuwa mwalimu mkuu ndiye kichocheo cha huo mchango na yeye ndiye anasimamia hafai na kwa tamko la Rais hana kazi.

Mkuu wa Mkoa aliwataka walimu hao kuacha kuchezea maagizo ya serikali. Aidha, alionesha kuwashangaa waratibu wa elimu ambao katika maeneo yao kuna michango inayoendelea na wao hawafahamu. Aidha, aliwaelekeza waratibu hao kuwepo katika vikao vya bodi na kamati za shule ili kufahamu hli ya mambo inavyokwenda.
=30=

No comments:

Post a Comment