Saturday, January 1, 2011

...MAISHA BORA YANATOKANA NA KUFANYA KAZI KWA JUHUDI NA MAARIFA!

Wananchi wamekumbushwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujiletea maisha bora na si kutegemea kuwa maisha mazuri yanateremka kutoka juu.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Bibi Evarista Kalalu katika hafla fupi ya kukabidhi mkopo wa zana za kilimo trekta kubwa manane na ndogo 25 uliotolewa na Idodi SACCOS iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya Idodi SACCOS zilizopo katika Kata ya Idodi, Tarafa ya Idodi katika  Halmashauri ya Iringa.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu akikabidhi mkopo wa Trekta

Bibi Kalalu amesema kuwa maisha rahasi kwa jamii yanatengenezwa kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na si kukaa na kusubiri muujiza kutoka juu. Ameongeza kuwa vijana wengi wamekimbilia maisha wanayodhani ni rahisi hasa mijini na kujikuta wanaharibikiwa na kupoteza muelekeo hivyo kuagiza vijana washawishiwe kutokimbilia maisha hayo na wajiingize katika kilimo na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS). Ametanabaisha kuwa usalama wa Tarafa ya Idodi na Mkoa wa Iringa utatokana na kushawishiwa huko kwa vijana kufanya kazi mbalimbali na si kupoteza muda na muelekeo katika maisha.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amefafanua madhumuni ya kuanzisha vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) mwanzoni mwa miaka ya 2000 kuwa ni mkakati wa serikali kuwakomboa wananchi wake. Amesema “nguvu za wananchi zikiwekwa pamoja kwa malengo mahususi unakuwa ni mtaji mkubwa sana” hivyo kuwataka wananchi wengi zaidi kujiunga katika vyama vya akiba na mikopo ili kuunganisha nguvu zao. Amesema “wanaidodi wengine wasio wanachama wawe tayari kujifunza na kujiunga kutoka SACCOS”.

Alichukua nafasi hiyo kuzitaka kata nyingine kubuni bidhaa nyingine isiyopatikana katika Kata ya Idodi ili kuongeza wigo wa utoaji huduma katika Tarafa mzima ya Idodi jambo litakalodumisha ushirikiano na udugu.  

Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Lucy Nyallu amesema kuwa kilimo cha kisasa hakitegemei kubahatisha bali kinategemea matumizi sahihi ya mbolea, uchaguzi wa mbegu bora na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa kilimo.

Mwenyekiti wa SACCOS hiyo Ngoola Mwangosi amezitaja changamoto zinazoikabili SACCOS hiyo kuwa ni pamoja na wadau wa mikopo ya stakabadhi mazao kutotoa mikopo ya kukopesha kwa wakati, na baadhi ya wanancha kutorejesha mikopo kwa wakati. Ameitaja changamoto nyingine kuwa ni wananchama kutokuwa na zana za kisasa za kilimo na kusababisha uzalishaji duni.

Chama cha ushirika wa akiba na mikopo (Idodi SACCOS DYK) kilisajiliwa rasmi Disemba, 2004 kikiwa na wanachama 178 na vikundi vya wajasiliamali sita kikiwa na hisa zenye thamani ya Tsh. 3,600,000, akiba Tsh. 107,286,400 na amana Tsh. 7,200,000.

No comments:

Post a Comment