Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi
wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) wametakiwa kusoma kwa juhudi
na maarifa na kuacha utukutu ili wawe raia wenye mchango kwa Taifa lao.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipofanya ziara
ya kutembelea wanufaika wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa.
Ayubu
alisema “serikali tunategemea msome kwa
bidii sana na msiwe watukutu. Nia ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais Dr. John Magufuli ni kujenga msingi imara kwa wananchi wake kupitia elimu.
Tunataka kuwa na Taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi na
kujitegemea”.
Alisema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kupata elimu
bila malipo na fedha kupitia TASAF kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya
shule.
Katibu
Tawala Mkoa, alisema kuwa wapo wazazi wanaozembea kuwanunulia watoto wao
wanufaika wa TASAF wafuatiliwe ili waweze kutimiza wajibu huo. Alisema kuwa
lengo la fedha hizo ni kuwawezesha watoto hao kupata sare za shule, madaftari,
kalamu na mahitaji mengine muhimu ya shule.
“Hapa lazima ifahamike kuwa, fedha hizi si za wazazi wla walezi, ni
fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanufaika kupata mahitaji yao ya lazima
kwa ajili ya shule ili wasijisikie wanyonge pindi wanapokuwa shuleni”
alisisitiza Ayubu.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi
wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza
changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF
Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
No comments:
Post a Comment