Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanufaika
wa mpango wa kunusuru kaya masikini mkoani Iringa wametakiwa kuzingatia suala
la lishe wakati wanawake wanapokuwa wajawazito na wanapojifungua ili kuwa na
watoto wenye hali nzuri ya lishe.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea
na wanufaika wa mpango wa TASAF na kamati ya usimamizi ngazi ya jamii
alipotembelea wanufaika wa elimu wa mpango wa TASAF katika Kata ya Kitwiru Manispaa
ya Iringa hivi karibuni.
Ayubu
aliitaka kamati ya usimamizi ngazi ya jamii na serikali ya kijiji kuwasisitiza
wanufaika waa TASAF wanapokuwa wajawazito kuhudhuria vituo vya afya ili kupewa
elimu ya lishe. Alisema kuwa elimu ya lishe ni muhimu kwa makuzi ya mtoto tokea
akiwa tumboni kwa mama yake.
“Siku 1,000
ni muhimu sana kwa lishe katika mchango wa makuzi ya mtoto. Ukosefu wa lishe
husababisha kutokuwa vizuri na kudumaa kiakili” alisema Ayubu. Alisema kuwa
hali hiyo isipoangaliwa mapema inasababisha mzunguko wa umasikini katika
familia na jamii kwa ujumla. Aliwasisitiza wanufaika wa fedha za kliniki
kuhudhuria kliniki kwa sababu serikali imekopa fedha ili kunusuru wananchi wake
katika suala la lishe.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi
wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza
changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF
Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
No comments:
Post a Comment