Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mpango
wa kunusuru kaya masikini (TASAF) una lenga kuhakikisha wanafunzi wanufaika wa
mpango huo wanapata huduma za msingi zitakazowawezesha kusoma kwa bidii.
Kauli
hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea
na wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika shule ya msingi
Kibwabwa iliyopo Kata ya Kitwiru Manispaa ya Iringa hivi karibuni.
Ayubu
alisema kuwa serikali kupitia TASAF imelenga kumuwezesha mtoto wa kitanzania
kufikia malengo yake kupitia fursa ya elimu. Alisema kuwa kutokana na umuhimu
wa elimu kwa wananchi, serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dr.
John Magufuli iliamua kutoa elimu bila malipo ili watoto wote wa kitanzania wapate
fursa hiyo.
“Kupitia mpango wa TASAF,
serikali inatoa fedha ili wanafunzi wanaotoka katika kaya zisizo na uwezo
waweze kugharamia mahitaji ya muhimu kwa mwanafunzi. Mahitaji hayo ni sare,
viatu, madaftari, kalamu na masweta ili kujikinga na baridi” alisema Ayubu.
Wakati
huohuo, Katibu Tawala Mkoa aliwashukuru kamati ya usimamizi ngazi ya jamii (CMC)
kwa kazi nzuri kuwasimamia wanufaika katika kufikia malengo ya mpango wa TASAF.
“Tuendelee kusimamia vizuri ili kuleta
mafanikio yaliyokusudiwa. Lazima kuwakumbusha wanufaika kuwa pesa za TASAF si
za burebure, serikali inaona wananchi wake wanakosa baadhi ya mahitaji ya
msingi, hivyo fedha hiyo ni kwa ajili ya kusaidia kufikia mahitaji hayo”
alisema Ayubu.
Katibu
Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika
wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto
zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa
mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
No comments:
Post a Comment