Wednesday, July 27, 2011

WATUMISHI WA RAS IRINGA WAPEWA SOMO LA RUSHWA 

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ilianzisha Mkakati wa kudhibiti Rushwa mahali pa kazi ili Ofisi hiyo iwe ni eneo salama kutolea huduma kwa wananchi.
Paulos Lekamoi, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa


Hayo yamesemwa na Mwanansheria wa Ofisi hiyo, Paulos Lekamoi wakati akiwasilisha mada juu ya Sheria ya Rushwa na Wajibu wa Watumishi wa Umma katika kudhibiti vitendo vya rushwa katika ukumbi wa Chuo kikuu Huria Tanzania tawi la Iringa katika Manispaa ya Iringa.

Lekamoi amesema “katika kuhakikisha rushwa mahali pa kazi haina nafasi ilianzisha mkakati wa kudhibiti rushwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa”.

Amesema mkakati huo umezingatia mkakati wa kitaifa wa kudhibiti rushwa ambapo lengo kuu ni kuimarisha njia za kupambana na rushwa, kuweka mifumo ya uadilifu, uwajibikaji na uwazi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na uzingatiaji wa Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007.

Lekamoi amesema katika sehemu ya III ya Sheria Na. 11 imeleta mabadiliko makubwa sana yanayoenda sambamba na Azimio la Umoja wa Mataifa la Mwaka 2005. Amesema Sheria hii imeongeza makosa yaliyopo kwenye Sura ya 329 ya Sheria kama ilivyorekebishwa Mwaka 2000 na kuyataja baadhi ya makosa kuwa ni mchakato wa rushwa (kifungu cha 4), kutumia nyaraka mbalimbali kumpotosha msimamizi (kifungu cha 6), Maafisa wa Serikali kutumia madaraka yao kujinufaisha (kifungu cha 7), kupatikana na mali yoyote ambayo imepatikana kwa njia ya Rushwa (kifungu cha 10).

Amesema kifungu cha 15 (i) (a) na (b) cha Sheria Na. 11, 2007 kinazungunzia makosa yanayohusu upokeaji wa rushwa ambapo Mtumishi wa Umma anaweza kujikuta amejiingiza aidha kwa kujua au kwa kutojua.

Ameyataja makosa hayo kuwa ni kushirikiana na mtu mwingine au mtumishi mwenyewe kushawishi kupokea au kukubalikupokea chochote kwa manufaa yake ili kutekeleza lengo lolote ambalo kimsingi anatakiwa alifanye katika shughuli zake za kila siku.

Vilevile, kifungu Na. 15 (a) kinamtia hatiani mtu yeyote atakaetoa ahadi ya kumpendelea mtu yeyote.


No comments:

Post a Comment