Jamii
imetakiwa kubalidilika na kupinga vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa wanawake
na watoto wa kike nchini kwa kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika
kuhamasisha usawa wa kijinsia.
Kauli
hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika
hotuba yake ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kimkoa
katika kijiji cha Ibangamoyo, Kata ya Ulanda Wilayani Iringa leo.
Dkt.
Christine amesema kuwa ”napenda kutoa wito kwa jamii mzima kubadili mitazamo iliyopitwa
na wakati dhidi ya wanawake kwa sababu haina nafasi kwa wakati tulionao sasa.
Ni lazima sote kwa pamoja tufahamu kuwa kila mtu anaweza, awe mwanamke au
mwanaume”. Amesema kuwa lazima vitendo vya dhuluma dhidi ya wanawake na watoto
wa kike vikemewe vikali na kuhimiza matumizi ya sheria na haki katika kupinga
unyanyasaji na dhuluma wanazofanyiwa wanawake. Amesema ”hapo nyuma wanawake
waliachwa nyuma kwa mengi ya muhimu kama elimu, ajira, mitaji na katika kutoa
maamuzi lakini sasa umefika wakati wa kutambua uwezo na mahitaji yao katika
kuendeleza gurudumu la maendeleo katika jamii”.
Akiongelea
nafasi ya Serikali katika kuhakikisha wanawake wanapatiwa haki katika masuala
mbalimbali ya kijamii na kiuchumi amesema ”Serikali imeweka mikakati mizuri
sana ya kuwawezesha wanawake katika masuala
ya elimu, ajira, nafasi za uongozi lakini tatizo limebaki katika ngazi
ya familia, vijiji na Kata”. Aidha, ameshauri kuwekwa mfumo mzuri wa
kushughulikia matatizo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na kuweka vizuri
kumbukumbu za matukio hayo ili tuweze kuwa na kumbukumbu sahihi.
Katika
kusisitiza hilo, ameziagiza Halmashauri za za Wilaya na Manispaa kuhakikisha
matatizo yanayotokana na unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanashugulikiwa
vizuri na kutunza kumbukumbu za matukio hayo kuanzia ngazi za vijiji, Kata hadi
Halmashauri za Wilaya. Amewataka kuwa na rejesta inayoorodhesha matukio yote ya
ukatili wa kijinsia na jinsi matukio hayo yalivyoshughulikiwa katika ngazi
husika. Kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi hata kuweza kufanya tafiti ili kujua
ukubwa wa tatizo hilo katika ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Dkt.
Christine ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kuhakikisha elimu
inatolewa mara kwa mara katika vijiji vyote ili kila mtu aelewe madhara ya
ukatili wa kijinsia na pale itakapotokea mtu kufanya unyanyasaji huo achukuliwe
hatua zinazostahili na wale wote wanaotendewa ukatili waweze kupata haki zao.
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa Mkoa wa Iringa hauwezi kupiga hatua zaidi katika
maendeleo iliwa wanawake hawatapewa nafasi katika nyanja za kiuchumi, kisiasa
na kijamii. Amesema ”ili Mkoa wetu wa Iringa uweze kupiga hatua zaidi katika
maendeleo ni lazima wanawake wapewe nafasi katika nyanja za Kuchumi, Kisiasa na
Kijamii”. Aidha, amesisitiza elimu lazima iendelee kutolewa kwa wananchi wote
na kwa muda wote siyo tu kusubiri katika kipindi cha maadhimisho hayo.
Maadhimisho
ya siku ya wanawake duniani yanaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘uelewa wa masuala ya jinsia; ongeza kasi’ kwa lengo la kuweka msisitizo
kwa jamii kuona umuhimu wa kila mmoja wetu kuelewa maana ya usawa wa jinsia una
umuhimu wake katika jamii.
Maadhimisho
haya ni matokeo ya kumbukumbu ya kihistoria ya mwanaharakati mwanamke wa nchini Ujerumani Clara Serkin aliyejaliwa ujasiri na ushupavu wa kutetea wanawake
dhidi ya kandamizwaji, unyanyaswaji na
dhuluma walizokuwa wakifanyiwa na wanaume katika nyanja za kiuchumi, kisiasa,
kijamii na kiutamaduni.
Katika
taarifa ya maendeleo ya shughuli za wanawake wa Wilaya ya Iringa
iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya
Wanawake Duniani Immaculate Senje amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa imekuwa ikihamasisha wanawake kujiunga katika vikundi na kupatiwa elimu
ya ujasiliamali na jinsi ya kubuni miradi ya maendeleo na jinsi ya kuiendesha.
Amesema kuwa hadi sasa jumla ya vikundi 176 ambavyo kati ya vikundi hivyo vikundi 100 ni vya kawaida
na vikundi 66 ni benki za kijamii. Amesema kuwa vikundi hivyo vina jumla
wanachama 2,021.
Amesema
kuwa Halmashauri yake imekuwa ikihamasisha kuunda benki za kijamii vijijini
(VICOBA), ambapo jumla ya VICOBA 66 vimeanzishwa vikiwa na wanachama 1361 na
mtaji wa sh. 150,980,560. Aidha, amesema kuwa wanawake wamekuwa wakihamasishwa
kujiunga na SACCOS katika maeneo yao kwa malengo ya kujijengea tabia ya kukopa
na kuweka. Amesema jumla ya wanawake 1,527 sawa na asilimia 40 wamejiunga na SACCOS.
Akiongelea
umiki wa ardhi, Immaculate amesema kuwa Halmashauri imeendelea na jitihada za
kuwapa fursa wanawake ya kumiliki ardhi kwa sababu ndiyo rasilimali pekee
inayoweza kumkomboa mwanamke kuondokana na umasikini. Amesema kuwa bado hakuna
usawa katika umiliki wa ardhi kati ya wanawake na wanaume. Amesema kuwa kati ya
watu 6,133 waliopata hati za kimila za kumiliki ardhi wanawake 2,006 wamepata
hati za kumiliko ardhi.
=30=
No comments:
Post a Comment