Serikali inatambua na kuthamini
mchango wa vyombo vya habari nchini katika kuhabarisha na kuhamasisha jamii
katika kufanikisha kampeni za afya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Gloria Tesha
alipokuwa akitoa mada juu ya majukumu ya vyombo vya habari katika huduma za
chanjo nchini katika ukumbi wa Chuo kikuu Hurua tawi la Iringa.
Gloria amesema “vyombo vya habari
vina uwezo na ushawishi mkubwa katika kuhamasisha jamii kupitia mfumo na
uongozi uliopo kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa katika mikakati yote ya
maendeleo ya nchi ikiwemo huduma za afya”.
Amesema kuwa uwezo wa vyombo vya
habari umejidhihirisha katika kutoa habari sahihi na muhimu kwa muda muafaka
kwa jamii kwa lengo la kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha wananchi
kushiriki katika huduma na kampeni mbalimbali. “Habari zinaiwezesha jamii
kufahamu mambo mbalimbali na kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi”
alisisitiza Gloria.
Akielezea mchango wa vyombo vya
habari katika kufanikisha kampeni za afya, amesema kuwa ushiriki wa vyombo vya
habari katika uanzishwaji wa chanjo mpya ni nyenzo muhimu katika mchakato mzima
wa kuboresha afya ya watoto nchini na kufikia malengo ya milenia. Amesema dhana
hii inakubalika kutokana na ukweli ulivyo kulingana na historia ya mchango wa
vyombo vya habari ilivyo katika maendeleo ya Tanzania. Amesema Wizara inategemea
kuwa vyombo vya habari vitawakilisha ujumbe kwa jamii katika uanzishwaji wa chanjo
mpya; pamoja na lengo la nne la milenia linalolenga kupunguza vifo vya watoto
chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili ifikapo 2015.
Kuhusu ujumbe kwa jamii kupitia vyombo
vya habari juu ya chanjo ya Rotavirus amesema magonjwa ya kuharisha husababishwa na
vimelea vya aina mbalimbali lakini virusi vya Rota huchangia kwa kiwango
kikubwa katika magonjwa ya kuharisha kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka
mitano. Amesema virusi vya Rota huenezwa kwa njia ya kula na /au kunywa maji
yaliyochafuliwa na kinyesi chenye virusi hivyo.
Amesema kuwa dalili kuu za ugonjwa
huo ni kutapika na kuharisha na mara nyingine huambatana na homa. Ameongeza
kuharisha huchukua kati ya siku 4 hadi 7 sambamba na upungufu wa maji mwilini.
Mtoa mada huyo ameelezea njia za
kujikinga kuwa ni kumnyoshesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya
mwanzo tangu anapozaliwa bila kumpa kitu chochote kingine chochote yakiwemo
maji. Kinga nyingine ameitaja kuwa ni usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa
maji safi na sabuni husaidia kupunguza maambukizo ya magonjwa ya kuharisha kwa
ujumla. Aidha, amesisitiza kuwa wazazi na walezi ni vizuri wafuate ratiba ili
watoto wasipitishe umri wa kupata dozi ya chanjo ya Rotavirus kwasababu umri
ukizidi ataikosa chanjo hiyo na wazazi na walezi watapewa tarehe ya kurudi tena
wiki nne baada ya dozi ya kwanza.
Akielezea mategemeo ya Wizara baada ya semina hiyo
kwa waandishi wa habari, Gloria amesema kuwa anategemea kuwa waandishi wa
habari wataweka habari za chanjo hiyo
kuwa habari kuu kwa sababu inahusu kunusuru watoto na vifo vinavyozuilika.
Amesema pia anategemea kupata habari nyingi katika makala, habari, majarida na
vipindi vya kutosha vya kuelimisha jamii.
=30=
No comments:
Post a Comment