RAIS KIKWETE
AHUTUBIA WANANCHI KUPITIA BUNGE LA JAMHURI
Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa
Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa
Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa
Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa
Wabunge;
Mabibi
na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu
ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa
uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa
Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja
kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache
zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni
Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja
kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea kasoro
zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na wapo pia
waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya Tanzania katika
Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika
Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja
na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye
hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya,
napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama
mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya
mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia
walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya
Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya
Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya
hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.
Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa
marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum
ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo
itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili
ya Katiba ifanyike na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na
wananchi katika Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa
tumepata Katiba Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya
tafakuri na tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni
kufanyika kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa
Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na
wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia
kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti
inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000.
Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980
ilipofika mwaka 1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000
tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha
Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni
marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na
uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya
kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu
nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society
ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye
sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali
halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009
kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na
kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya
meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko
duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na
Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe
za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya pembe za
ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978 vilikamatwa. Aidha,
katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu vilivyotokea
Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797 vilikamatwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na
faru lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi
za Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe,
Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo
limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua
kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa
ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua
thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi
kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au
faru atakayeuawa.
Mheshimiwa
Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi
wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa
yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani
kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni
sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini.
Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia
itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia
kazi. Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa
kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu
na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za
kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa
mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo
iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa
wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo
zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na
hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za
wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi
tunaowaongoza wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za
nchi. Naomba pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na
kukutwa katika maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria.
Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya.
Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo
tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi
kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza
nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo
imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali
maombi kama hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni
miezi saba (tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa
wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya
juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa
Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO)
na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili.
Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi
majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami
tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo
kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona
Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi
yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua
hatua za kufanya amani ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia
nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya
hivyo. Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi
ya watu au vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la
kwanza, wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha
au kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini
ya utaratibu huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi
kama hapana budi kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na
kwa ujasiri mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana
wetu watatu shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa
wetu hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika,
napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi
dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri
katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga
mahusiano mapya miongoni mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana
wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya
iliyowezesha mafanikio kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika
Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi
Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba
kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu
ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo lililonileta
hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na
nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo kutokana na
maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni
ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda,
Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na
Burundi. Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe
24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa,
Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi
hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo
mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi
zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama
zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za
Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa
msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia,
tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe
na ruhusa imetolewa kwa nchi yo yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake
au kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano
hiyo, kuna mambo yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na
nchi hizo kwa lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1)
Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala,
Kigali na Bujumbura.
(2)
Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na
Sudani ya Kusini.
(3)
Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4)
Kuanzisha
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kutekeleza vipengele vyote;
(5)
Kuharakisha
Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba
ya Shirikisho.
(6)
Kuharakisha
uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single
East African Community Tourist Visa);
(7)
Kuandaa
utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi
zao; na
(8)
Kuongeza
uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na
yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane
hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji
wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya
nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la
kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe
kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania
katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo
sote ni wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha
kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya
Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine.
Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba
sasa tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki
katika ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la
mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo
linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili
kuwezesha mafuta yao kufika kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa
Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na
Burundi kuwa nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa
Tanzania. Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa
katika ujenzi wa bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya
kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna
tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo
chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua
ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini
kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha
juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya
pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road
Network, na tuna Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli
ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli
hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia
mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki
ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya
wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na
tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi.
Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013
walipokutana kuamua kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika
Mashariki kwa kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne
yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa utekelezaji na
Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo. Mambo hayo ni
matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa ya Pamoja ya
Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa tayari
waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru wa
Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani
wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano
Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012
Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya
Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo
hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na kukusanya
mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa zinazopitia nchi
moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa mapato
utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia. Mapato hayo
yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka
mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la
Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano wa
15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza
kutekeleza? Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la
Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii ya Himaya ya
Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi wanachama
uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya hatua
iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho.
Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi
wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine
yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri
litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa
Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha
mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza maswali
mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi wenzangu
watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu wamekosa
imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao? Je
wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au
sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa
hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa).
Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya
jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote mwanachama. Na ukweli
ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu kwa Jumuiya.
Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na kushiriki kwa ukamilifu katika
ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya
wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini
wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari
tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the
Willing). Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?)
Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo
wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko
tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli.
Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti
kwamba Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano
wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa
kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania
tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo
Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa
yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa
Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo
hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha
ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na
Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano
wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo
kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda mrefu
kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa
Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo
jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo
kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele
cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu
na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa
ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na
ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli
akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi
msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira,
uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu.
Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba
kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende
hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa
tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge
Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba
ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi
ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya
kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la
Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho
la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa
nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi
huo si mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko
la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na
kunufaisha wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue
ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha nchi kujiunga na
kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo ya kiuchumi
yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi imara kwa
Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu za awali
hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki ipasavyo,
Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya
zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano zitekelezwe moja
baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa msimamo na mtazamo wetu,
Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo siyo msimamo wangu au
wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio wengi.
Bila ya shaka sote
tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati
Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha
Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na
Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwa asilimia
74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia25.4
tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi
zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa Shirikisho na
kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana wanaunga mkono kuwepo kwa
Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo lisifanywe haraka
haraka. Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua
kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda sambamba na ile ya
wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki mapendekezo ya Kamati ile ya
mwaka 2004 iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos Wako wakati ule akiwa
Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa kupendekeza namna ya
kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha
lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa
nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na
mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya
kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama
kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania
kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za Watanzania kuhusu
ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo yabaki kwenye mamlaka ya nchi
wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa utengamano Kamati ilipendekeza
kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo
wake wa miaka mitano. Baada ya hapo muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata
unaweza kupunguzwa. Kwa mfano walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda
Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho
ili mara wakati huo ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara
baada ya ngazi hiyo kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha
yanaanza. Ngazi hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza.
Kamati pia imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho
kwamba wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata
mapendekezo ya Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa
Tanzania haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa
na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya yao
inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano kuhusu mambo
yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi pale watu
wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa Jumuiya na
Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui mambo
yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika
Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa
vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika
nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha
mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua
tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa
imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki
katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa
Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa
Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe
hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.
Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya ya
Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo
yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa
kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi
wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
No comments:
Post a Comment