Jamii imetakiwa
kutenga muda wa kuwasaidia watoto walio katika mazingira magumu ili kuwatia
moyo na kuwasaidia kufikia malengo yao.
Mkuu wa Kituo cha Amani, Mama Erica Mwakalebela
Kauli hiyo
imetolewa na Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Amani kilichopo
wilayani Kilolo Erica Mwakalebela alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya kituo
kwa akina mama wa kikundi cha Songambele chenye makazi yake Manispaa ya Iringa
walipotembelea kituo hicho kuongea na watoto na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Erica amesema
kuwa watoto yatima wanahitaji kusaidiwa kwa hali na mali. Amesema “hatuwezi
kuwa wakamilifu kama hatutatoa muda wetu kuwasaidia watoto yatima. Watoto hawa
ni wetu hivyo jukumu la kuwahudumia ni letu sote”. Ametoa rai kwa jamii mzima
kutenga muda na rasilimali kuwahudumia watoto yatina na watoto walio katika
mazingira magumu. Amesema kuwa watoto yatima kama walivyo watoto wengine
wanamalengo mbalimbali katika maisha yao ambayo ili waweze kuyatimiza ni lazima
jamii iweze kuwasaidia kuyafikia. Amesema kuwa kuwawezesha kuyafikia malengo
hayo kutawasaidia kutimiza jukumu lao katika ujenzi wa familia zao na Taifa kwa
ujumla.
Akiongelea
mafanikio ya kituo hicho, mkuu wa kituo hicho ameyataja kuwa ni kuwalea na
kuwasomesha watoto katika hatua mbalimbali kuanzia shule ya msingi, sekondari,
vyuo vya ufundi, utalii hadi chuo kikuu. Ameyataja mafanikio mengine kuwa ni
kuwasaidia watoto katika kituo hicho hadi kupata ajira kwa wale waliokamilisha
masomo yao. Aidha, amesema kuwa kituo hicho kimekuwa kikiajiri pia watoto
wanaofanya vizuri katika masomo yao na fani mbalimbali katika miradi
inayoendeshwa kituoni hapo.
Erica amezitaja
baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo chake kuwa ni elimu, chakula na ajira
kwa watoto hao. Aidha, ametoa wito kwa wafadhili na wadau wengine kujitokeza na
kukisaidia kituo hicho katika kukabiliana na changamoto hizo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Songambele, Mama Rehema Dunga
Akitoa nasaha
zake kwa watoto yatima wa kituo cha Amani, Mwenyekiti wa kikundi cha kinamama
cha Songambele, Rehema Dunga amewataka watoto hao kutokukata tamaa katika maisha
yao na kusongambele. Akielezea lengo la kutembelea kituo hicho, Mwenyekiti wa
Songambele amesema kuwa lengo ni kukutana na kuzungumza na watoto hao ili
kuwasaidia kusongambele.
Amewataka watoto hao kuwa wasikivu na wenye kujituma
katika kile wanachofundishwa ili waweze kufanikiwa. “Wakinamama wa Songambele
tumekuja hapa kuwaonesha upendo na kuwatia moyo msirudi nyuma bali msongembele
katika kila jambo mnalolifanya katika maisha yenu” alisisitiza Rehema.
Katika ziara ya
kikundi hicho kwa kituo cha kulelea watoto yatima Amani, kinamama wa Songambele
walipika chakula cha mchana kwa watoto hao zaidi ya 100. Aidha, walipeleka
zawadi mbalimbali kama sabuni, madaftari, kalamu, mafuta, maji, juisi, dawa za
meno, miswaki pamoja na vitu vingine vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Tshs.
650,000/=
Miongoni mwa zawadi zilizotolewa na kinamama wa Songambele kwa kituo cha Amani
Kikundi cha
kinamama cha Songambele kilianzishwa miaka miwili iliyopita kwa lengo la
kuwawezesha kina mama na familia zao kusonga mbele kimaendeleo. Kikundi kina wanachama
24 kikiwa na makao makuu eneo la Lugalo, Manispaa ya Iringa.
Kinamama wa Songambele
Kinamama wa Songambele wakiwa katika Pozi la pamoja
=30=
No comments:
Post a Comment