Serikali
inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na wananchi wa Italia katika
kuboresha huduma za matibabu kwa watoto kwa lengo la kupunguza vifo vya watoto.
Kauli
hiyo imetolewa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete katika hotuba yake kwenye
uzinduzi wa jengo la huduma za watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Iringa.
Mama Salma Kikwete akizindua jengo la Watoto
Mama
Salma amesema “tupo hapa kuzindua jengo la kutolea huduma za watoto. Lakini
kabla ya kuzindua jengo hili, naomba niwashukuru sana serikali ya Italia kwa msaada
waliotoa kulijenga jengo wa Tshs. 1,842,000,000”. Amesema kuwa serikali ya
Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa waliotoa wananchi wa Italia kwa
wananchi wa Tanzania. “Kwa mchango huu, wananchi wa Italia wametambua umuhimu
wa kuboresha huduma za matibabu kwa watoto, ambazo zitasaidia kupunguza vifo
vya watoto” alisisitiza Mama Salma. Ameongeza kuwa jengo hilo litapunguza
msongamano wa watoto wagonjwa wodini na kuboresha huduma za afya ya watoto
katika hospitali ya rufaa ya mkoa.
Akiongelea
uhusiano kati ya hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na hospitali ya Vicenza
ya mkoa wa Veneto nchini Italia Mama Salma amesema kuwa uhusiano huo unapaswa
kuimarishwa na kuheshimiwa kwa sababu unaboresha utoaji wa huduma za afya
katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
Kutokana
na hospitali nyingi kulalamikiwa kuhusu utoaji huduma usiridhisha, Mama Salma
ameitaka hospitali ya rufaa ya mkoa kuwa mfano katika utoaji huduma bora kwa
wananchi. Amewataka madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kutoa huduma kwa
kujituma, uadilifu, uzalendo na kutumia lugha rafiki inayoweza kumfariji
mgonjwa.
Akiwasilisha
taarifa ya mradi wa kuboresha huduma za mama na mtoto inayohusisha ujenzi wa
jengo la kujifungulia mama wajawazito na ujenzi wa wodi ya watoto katika hospitali
ya rufaa ya mkoa, mganga mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Robert Salim amesema
kuwa lengo la mradi ni kuboresha huduma za kujifungua, kupunguza vifo vya
wajawazito na vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na baridi, kukosa hewa
na kupunguza msongamano. Amesema mradi huo pia utapunguza maambukizi ya
magonjwa kwa mama waliojifungua na kuboresha utoaji wa huduma kwa urahisi kwa
mama wajawazito wanaojifungua wanaojifungua kwa kuwa na eneo kubwa la
kufanyia kazi.
Dk.
Salim amesema kuwa kutokana na kuongezeka kwa magonjwa ya kuambukiza na vifo
vya watoto chini ya miaka mitano, msongamato katika wodi ya watoto,
kukosekana kwa chumba cha kuhudumia watoto walio mahututi, chumba cha
kuhudumia watoto njiti na wenye utapia mlo mkali, ofisi ya mkuu wa mkoa wa
Iringa kwa kushirikiana na hospitali rafiki ya Vicenza ya Italia iliona ni
vema kuwa na wodi maalumu kwa ajili ya kuwahudumia watoto katika hospitali ya
rufaa ya mkoa.
=30=
|
|
|
No comments:
Post a Comment