MKUU wa Mkoa wa Iringa amewaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri mchakato wa vocha za pembejeo za kilimo kwa kutokuwafumbia macho mawakala wababaishaji na wanaojinufaisha kupitia migongo ya wakulima ili kuondoa manung’uniko na wakulima kunufaika na mfumo huu wa vocha za ruzuku za serikali.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma
Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kamati ya vocha za pembejeo ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika kikao cha kamati ya vocha za pembejeo mkoa wa Iringa kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Dk. Ishengoma amesema “ili kuhakikisha usimamiaji wa vocha hizo za pembejeo unakuwa madhubuti, ni lazima wakuu wa Wilaya kusimamia vizuri mchakato mzima wa vocha katika wilaya zenu”. Aidha, amewataka Wakuu hao wa Wilaya kutokuwafumbia macho mawakala wasio na vigezo ili huduma hiyo iweze kufanikiwa na kuwanufaisha wananchi kama yalivyo madhumuni ya Serikali.
Amesema “mfumo huu wa vocha ni mzuri sana ila una mianya ya rushwa hivyo tusichague mawakala matapeli bali tuchague mawalaka wenye rekodi nzuri na wasio na madeni na wasio wababaishaji kwa sababu lengo la serikali ni kumsaidia mkulima kwa kumpunguzia gharama katika pembejeo za kilimo” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu wa Mkoa aliagiza kamati ya vocha ya Wilaya na Wataalam wa kilimo kuwaelimisha wakulima juu ya utaratibu wa awali wa kufikisha pembejeo kwa wakulima kulingana na fomu zalizowasilishwa ma Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Akiwasilisha mapendekezo ya mgao wa vocha za pembejeo za kilimo kwa kila Halmashauri kwa msimu wa mwaka 2011/2012 katika kamati ya vocha ya Mkoa wa Iringa, Afisa Kilimo Mkuu katika Ofisi ya Mkuu Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni ameyataja mapendekezo hayo kwa kila Halmashauri kuwa ni Mufindi (kupandia 44,300, kukuzia 44,300, chotara 44,000, mpunga 300), Makete (kupandia 23,700, kukuzia 23,700, chotara 23,700), Iringa (kupandia 45,000, kukuzia 45,000, chotara 43,500, mpunga 2,500), Njombe Mji (kupandia 21,000, kukuzia 21,000, chotara 21,000), Manispaa (kupandia 4,000, kukuzia 4,000, chotara 4,000), Kilolo (kupandia 26,000, kukuzia 26,000, chotara 25,800, mpunga 200), Njombe (kupandia 42,500, kukuzia 42,500, chotara 42,500) na Ludewa (kupandia 24,500, kukuzia 24,500, chotara 24,000 na mpunga 500).
Akiongelea thamani za vocha moja moja msimu katika msimu wa mwaka 2011/ 2012 Nyoni amesema kuwa vocha za kupandia kilo 50 ni shilingi 28,000, kukuzia kilo 50 ni shilingi 18,500, mahindi chotara kilo 50 ni shilingi 20,000 na mpunga kilo 50 ni shilingi 12,000.
Nyoni amesema kuwa Mkoa unatarajia kupata mgao wa jumla ya vocha 693,000 za pembejeo za kilimo kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
No comments:
Post a Comment