Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanawake mkoani Iringa wametakiwa
kujitokeza kupima saratani ya mlango wa kizazi ili wanapogundulika na saratani
hiyo waanze matibabu mapema.
Wito huo umetolewa na mganga mkuu wa
mkoa wa Iringa, Dkt. Robert Salim alipokuwa akifungua semina ya kufuatilia
utekelezaji wa mipango na maazimio yaliyowekwa kuhusu kukabiliana na saratani
ya mlango wa kizazi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha afya ya msingi mjini
Iringa.
Dkt. Salim alisema kuwa saratani ya
mlango wa kizazi inasababisha maradhi na vifo kwa wanawake wengi nchini isipotambuliwa
na kuanza kutibiwa mapema. Alisema kuwa wanawake wote walioanza mahusiano ya
kimapenzi wanatakiwa kujitokeza katika vituo vya afya kupima ili
wanapogundulika wameathirika na saratani hiyo waanze tiba mapema. Alisema kuwa
yapo mahusiano makubwa baina ya maambukizi ya virusi vya ukimwi na saratani ya
mlango wa kizazi. Kutokana na mahusiano hayo ambayo kwayo mkoa wa Iringa
umeathirika sana na maambukizi ya ukimwi kwa 9.1% hivyo kusababisha ugonjwa wa
saratani ya mlango wa kizazi kuwa juu.
Nae Mkurugenzi wa uboreshaji afya
kutoka taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Dkt. Sarah Maongezi alisema kuwa
semina hiyo ililenga kufuatilia utekelezaji wa mipango na maazimio ya awali
waliyojiwekea katika kukabiliana na tatizo la saratani ya mlango wa kizazi
mkoani hapa. Alisema kwa kuwa mkoa wa Iringa ulianza muda mrefu mapambano dhidi
ya saratani ya mlango wa kizazi hivyo mkoa unatakiwa kuwa umepiga hatua za
mafanikio zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Alisema kuwa kwa hatua
iliyofikiwa na mkoa wa Iringa, mkoa huo unaweza kujihamasisha kununua vifaa na
vifaa tiba kwa lengo la kukabiliana na saratani ya mlango wa kizazi.
Saratani ya mlango wa kizazi ni
miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo kwa wanawake wengi ikikadiriwa kuwa
zaidi ya wanawake 4,000 hupoteza maisha nchini kila mwaka.
=30=
No comments:
Post a Comment