Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umejipanga kukabiliana
na watumishi feki katika sekta ya afya ili kutoa huduma za kitaalam kwa
wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala
Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akiongea na vyombo vya habari juu ya
mkoa ulivyojipanga kukabiliana na changamoto ya watumishi wasio na sifa katika
sekta ya afya mkoani hapa kufuatia wimbi la watumishi wasio na sifa kubainika
wakitoa huduma katika hospitali za serikali.
Ayubu alisema kuwa mkoa wa Iringa upo
makini kimfumo na rasilimali watu kukabiliana na tatizo la watumishi feki.
Alisema mifumo ya kuhakiki watumishi imeboreshwa zaidi katika miaka ya hivi
karibuni kwa lengo la kukabiliana na watumishi feki.
“Mtumishi yeyote anapoajiliwa
anawasilisha vyeti vyake vya kitaaluma alivyonavyo na vinakaguliwa. Kutokana na
wimbi la kugushi vyeti, mkoa umepanua wigo kwa kushirikisha taasisi zote
zinazohusika na utoaji vyeti husika kama NECTA, NACTE, vyuo vikuu ili
wathibitishe uhalali wa vyeti hivyo”, alisisitiza Ayubu.
Aliongeza kuwa mfumo wa kieletroniki
wa malipo na mishahara ulioanza mwaka 2011, umeongeza ufanisi katika udhibiti
wa vyeti feki kwa sababu mfumo unaingiza vyeti vyote kasha vinaenda kuhakikiwa
Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Alisema kuwa pamoja na kusaidia kubaini
watumishi wenye vyeti feki chini mfumo huo umeondoa tatizo la watumishi kulipwa
zaidi ya mara moja na kuondoa changamoto ya mishahara hewa. Katika mfumo huu
kama mtumishi alishaajiliwa serikalini mfumo utamgundua kirahisi hivyo kuwa
vigumu kulipwa mshahara zaidi ya mmoja. Alisema kuwa hata ule mchezo wa watu
kutumia vyeti vya watu wengine unapatiwa tiba.
Ayubu aliongeza kuwa watumishi wote
wa serikali wanavaa vitambulisho vya vya kazi vinavyomtambulisha jina kamili na
cheo ili iwe rahisi kwa anayepewa huduma kumtambua mtoa huduma. Ameongeza
utaratibu huo unaondoa malalamiko kwa wananchi kwa sababu kila mtumishi
anafahamika kwa jina na cheo chake.
Ayubu alisema mwaka 2011 mkoa
ulifanya uhakiki wa taarifa za watumishi wa umma ili kubaini uwepo wa watumishi
hewa. Alisema kuwa anajivunia kutokuwepo kwa watumishi hewa na mishahara hewa.
Afisa utumishi katika ofisi ya mkuu
wa mkoa, Gasto Andongwisye alisema katika kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa na
watumishi wenye sifa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kudhibiti
mishahara hewa, ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia sehemu ya utawala na rasilimali
watu imeendelea kufanya uhakiki kila mwezi kwa watumishi na ‘payroll’.
Andongwisye aliongeza kuwa katika
kuhakikisha hakuna mtumishi mamluki anayejipenyeza katika hospitali za serikali
mkoani hapa na kutoa huduma, idara zote katika hospitali wamekuwa wakifanya
vikao vya kila siku kupeana taarifa za kazi na vikao vya watumishi wote kila
idara kwa lengo la kufahamiana na kujadili changamoto zilizopo.
=30=
No comments:
Post a Comment