Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umejitahidi kudhibiti
mimba kwa wasichana wa shule za msingi na kuongeza idadi ya wasichana
wanaomaliza elimu ya msingi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa
kamati ya mitihani mkoa wa Iringa, Mwl Euzebio Mtavangu alipokuwa akifafanua maandalizi
ya mkoa wa Iringa katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015
utakaofanyika kuanzia kesho nchini nzima.
Mwl Mtavangu ambaye pia ni Kaimu
afisa elimu wa mkoa wa Iringa alisema kuwa mwaka 2015 idadi ya wasichana
wanaomaliza elimu ya msingi ni kubwa ikilinganishwa na idadi ya wavulana
kutokana na mkoa kudhibiti tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike katika shule
za msingi. Alisema kuwa kati ya watahiniwa 21,323 wa kumaliza elimu ya msingi
mwaka 2015, wasichana ni 11,448 na wavulana ni 9,875. Alisema kuwa tofauti na
miaka ya nyuma ambayo idadi ya wasichana waliokuwa wakihitimu elimu ya msingi
ilikuwa ndogo kutokana na wasichana wengi kupata ujauzito na kushindwa kumaliza
elimu ya msingi. Alisema kwa kutambua umuhimu na nafasi ya mtoto wa kike katika
jamii, mkoa wa Iringa utaendelea kudhibiti mimba kwa wasichana ili wote waweze
kumaliza elimu ya msingi na kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa. Akifafanua
ongezeko hilo kwa kila halmashauri, alilitaja ongezeko hilo kwa kila halmashauri
kama ifuatavyo; Manispaa ya Iringa Wasichana (1,748) na wavulana (1,534),
halmashauri ya wilaya ya Iringa Wasichana (3,046) na wavulana (2,618),
halmashauri ya wilaya ya Kilolo wasichana (3,088) na wavulana (2,776) na
halmashauri ya wilaya ya Mufindi wasichana (3,566) na wavulana (2,947).
Mwl Mtavangu alisema kuwa jumla ya
shule 457 zitafanya mhihani huo kwa mkoa wa Iringa, ikiwa ni Manispaa ya Iringa
shule (41), halmashauri ya wilaya ya Iringa (142), halmashauri ya wilaya ya
Kilolo (106) na halmashauri ya wilaya ya Mufindi (168). Alisema kuwa katika
mtihani huo, jumla ya mikondo 977 katika shule hizo 457 itahusika ikiwa na
wasimamizi 977.
Aliwataja watahiniwa wengine kuwa ni watahiniwa
wasioona watano wasichana wakiwa watatu na wavulana wawili. Wengine ni
watahiniwa wenye uono hafifu 33, wasichana (18) na wavulana (15).
Kwa upande wa shule zenye mchepuo wa
kiingereza alisema kuwa shule hizo
zipo 10 zenye jumla ya watahiniwa 455, wasichana wakiwa 222 na wavulana 233.
Katika siku ya kwanza mitahani ya sayansi, hisabati na Kiswahili itafanyika
ikifuatiwa na mitihani ya kiingereza na maarifa ya jamii.
Akiongelea matarajio ya ufaulu kwa
mkoa wa Iringa, alisema kuwa mkoa unatarajia kupanda hadi nafasi ya pili
kitaifa kutoka nafasi ya nne ya mwaka 2014 huku watahiniwa wakitarajiwa kufaulu
kwa zaidi ya asilimia 75 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2014 wa asilimia
68.58. Ikumbukwe kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukishika kati ya nafasi ya tatu na
nne kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa miaka 18 mfululizo.
=30=
No comments:
Post a Comment