Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Menejimenti ya halmashauri ya wilaya
ya Iringa yatakiwa kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata mpango na bajeti wa mwaka
2015/2016 ili kutokujitengenezea madeni.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa
wa Iringa, bibi Amina Masenza wakati wa uvunjaji wa Baraza la Madiwani la
halmashauri ya wilaya ya Iringa lililofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.
Mkuu wa mkoa amewataka kuhakikisha
maamuzi yatakayofanywa baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Madiwani yanakuwa yale tu
yaliyo ndani ya mpango na bajeti ya halmashauri wa mwaka 2015/2016 kama
ilivyoidhinishwa na Baraza la Madiwani. Amewataka kutunza vizuri nyaraka zote
za maamuzi yatakayofanyika katika kipindichote baada ya Baraza hilo kuvunjwa. “Natambua
kuwa waheshimiwa madiwani wote na hata watendaji mnatambua kuwa wakati madiwani
watakuwa hawapo katika nafasi zao ndani ya halmashauri, maamuzi ambayo
yangefanywa na madiwani sasa yatafanywa na Kamati ya Menejimenti ya halmashauri
(CMT), wafanye maamuzi ya busara na yenye manufaa kwa halmashauri” alisema bibi
Masenza.
Amesema kuwa mkoa utaendelea kuwa
karibu na halmashauri kwa ushauri na ufuatiliaji wa masuala ya serikali za
mitaa. Aidha, amezitaka serikali za mitaa mkoani Iringa kuomba usaidizi
unaotakiwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya halmashauri.
Mkuu wa mkoa wa Iringa
amewahakikishia madiwani hao kuwa serikali itaendelea kujivunia michango yao
waliyoitoa na kuifanya halmashauri ya wilaya ya Iringa kuwa mfano kwa kuongoza
katika ukusanyaji wa mapato ya ndani mwaka 2013/2014, kupata hati safi, kuwa
mshindi wa mkoa katika mashindano ya nanenane kikanda yaliyofanyika mkoani
Mbeya mwaka jana na kuwa halmashauriya kwanza kimkoa katika mashindano ya
ukimbizaji Mwenge wa Uhuru mwaka jana.
Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Iringa, Stephen Mhapa amesema kuwa anajivunia uhusiano mzuri baina ya
baraza lake na watendaji wa halmashauri katika kufanikisha shughuli za
kuwahudumia wananchi. Ameitaka halmashauri kuongeza wigo wa ukusanyaji wa
mapato ya ndani ili kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema kuwa mapato ya ndani
ya halmashauri ndiyo msingi wa kuwaletea maendeleo wananchi kwa sababu mipango
na matumizi yake inaendana na mazingira halisi ya halmashauri.
=30=
No comments:
Post a Comment