Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mwenge wa Uhuru utaweka mawe ya
msingi, kukagua, kuzindua na kufungua miradi 35 yenye thamani ya shilingi
4,985,562,793 katika mkoa wa Iringa.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa mkoa
wa Iringa, Bibi Amina Masenza alipokuwa akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa
mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajab Rutengwe katika eneo la Ruaha Mbuyuni
wilayani kilolo.
Bibi. Masenza amesema “Mwenge wa
Uhuru katika mkoa wa Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na
kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 35 yote ikiwa na thamani ya shilingi
4,985,562,793 ambapo kati ya fedha hizo serikali kuu imechangia shilingi
2,193,787,197 halmashauri za wilaya na manispaa shilingi 1,191,486,781,
michango ya wananchi shilingi 1,158,299,859 na wadau wa maendeleo shilingi
441,988,956”. Amesema kuwa jumla ya miradi 6 itafunguliwa, miradi 18
itazinduliwa, miradi 5 itawekewa mawe ya msingi na miradi 6 itakaguliwa na Mwenge
wa Uhuru. Miradi hiyo inatokana na sekta za kilimo, mifugo, maji, maliasili,
ujenzi, barabara, afya, elimu na maendeleo ya jamii.
Amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru
mwaka huu zimebeba ujumbe usemao “tumia haki yako ya kidemokrasia; chini ya
kaulimbiu; jiandikishe na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2015. Amesema
kuwa ujumbe huo ni muhimu katika kipindi ambapo watanzania wanapaswa
kushikamana zaidi na kudumisha amani na utulivu licha ya tofauti za itikadi ya
vyama.
Amesema kuwa ujumbe maalumu
umeambatana na jumbe za kudumu nne ambazo ni mapambano dhidi ya rushwa,
mapambano dhidi ya dawa za kulevya, mapambano dhidi ya ukimwi na mapambano
dhidi ya malaria.
=30=
No comments:
Post a Comment