Thursday, June 6, 2013

DKT. ISHENGOMA AKEMEA KILIMO KANDO YA RUAHA




Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine Ishengoma amekemea tabia ya ulimaji kandokando ya mto Ruaha ili kukulinda na kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.

Kauli hiyo ameitoka katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa Hamza Ginga ambaye ni diwani wa Kata ya Kwakilosa katika kijiji cha Kiwere Wilayani Iringa.

Dkt. Christine amesema kuwa tatizo la ulimaji kandokando ya mto Ruaha na mito mingine ni chanzo cha uharibifu wa mazingira. Amesema kuwa maeneo ya kando kando ya mito katika wilaya zote mkoani Iringa yamevamiwa na watu ambao wamekuwa wakilima hadi kwenye kingo za mito.amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria zinazozuia ulimaji huo, bado utekelezaji wake ni hafifu. Aidha, katika kudhibiti uharibifu huo amezitaka Halmashauri kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu hao. 

Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri na vijiji kuhakikisha ulimaji kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji unaachwa mara moja. Amesema kuwa watu wanaolima kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji na maeneo mengine yaliyokatazwa kisheria wachukuliwe hatua za kisheria. Amesema kuwa tabia ya ulimaji wa vinyungu umechangia sana kupunguza maji katika mito kutokana na kupungua kwa akiba ya maji katika maeneo oevu. Amewataka wananchi kuzingatia sheria ya maji ambayo mtu haruhusiwi kulima karibu na kingo za mito katika umbali wa mita 100 kutoka kwenye kingo ya mto. 

Dkt. Christine amewaagiza wananchi kuhakikisha kuwa miti iliyopandwa inatunzwa na kuzuia moto kichaa kuchoma miti hiyo. Aidha, ameutaka uongozi wa wilaya kusimamia kwa umakini na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaobainika kujihusisha na uchomaji moto miti. Amewataka wananchi kuwajibika kuzuia misitu isiungue moto na kuhakikisha kuwa hakuna moto kichaa mahali popote.

Akiongelea vyanzo vya maji, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema “vyanzo vya maji ni urithi wa taifa kila mtanzania ana haki ya kufaidika na rasilimali hii. Hivyo kila mtanzania ana wajibika kutunza vyanzo vya maji”. Amewataka wale wote waliovamia vyanzo vya maji na kukata miti na kulima katika maeneo hayo  waondoke mara moja na Serikali za vijiji ziwachukulie hatua wavamizi hao. 

Siku ya mazingura duniani katika mkoa wa Iringa ilitanguliwa na shughuli mbalimbali zikiwemo kutoa mafunzo maalumu kuhusu vyanzo vya maji na elimu juu ya mpango wa usimamizi shirikishi wa misitu, kutoa elimu juu ya madhara ya uharibifu wa mazingira, kufanya kampeni za kuzuia ulimaji kandokando ya vyanzo vya majina kutengeneza barabara za moto kuzuia misitu ya asili na ya kupandwa kuungua.
=30=

No comments:

Post a Comment